1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani Syria wasema serikali imekiuka usitishaji mapigano

29 Februari 2016

Upinzani wa Syria unasema serikali inavuruga makubaliano ya kusitisha mapigano huku Ufaransa ikitaka taarifa za kina kuhusu mashambulizi yanayokiuka makubaliano yaliyoanza kutekeleza usiku wa Ijumaa iliyopita.

https://p.dw.com/p/1I4Ma
Syrien Kafr Hamra Luftangriffe in Aleppo trotz Feuerpause
Picha: picture-alliance/abaca

Afisa wa ngazi ya juu wa kundi la upinzani la Syria amesema juhudi za kwanza za kukomesha mapigano baada ya karibu miaka mitano ya vita ziko katika hatari ya kusambaratika kabisa kwa sababu ya mashambulizi ya vikosi vys serikali.

Mkuu wa kundi hilo lenye makao yake nchini Saudi Arabia, Assad al-Zoubi, alisema anaamini jumuiya ya kimataifa imeshindwa kabisa katika jitihada zake na sharti hatua zichukuliwe dhidi ya utawala wa Syria, bila kufafanua. Kiongozi huyo amesema haoni dalili za maandalizi ya mazungumzo ya amani ambayo Umoja wa Mataifa ulitaka kuyaitisha Machi 7.

Ufaransa leo imeitisha kikao cha mataifa yanayosimamia utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Syria. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Jean-Marc Ayrault, alisema, "Tumepokea taarifa zinazoashiria kwamba mashambulizi yakiwemo ya kutokea angani yamekuwa yakiendelea dhidi ya maeneo yanayodhibitiwa na makundi ya upinzani yenye msimamo wa wastani. Yote haya yanahitaji kuthibitishwa. Ufaransa kwa hiyo imetaka kundi linalosimamia usitishwaji mapigano likutane bila kuchelewa."

Akizungumza na waandishi wa habari katika afisi za baraza la haki za binaadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva leo, waziri Ayrault pia alisema mzozo wa Syria ni mtihani utakaotoa tathmini ikiwa juhudi zinazofanywa katika kuzilinda haki za binaadamu zinafaulu, na akakiri kwa sasa zinafeli.

Makubaliano yakiukwa

Kauli yake inakuja wakati makubaliano ya kusitisha makubaliano yaliyoafikiwa kati ya Marekani na Urusi na kuungwa mkono na Umoja wa Mataifa, yakiingia siku yake ya tatu na yakionekana kuheshimiwa, licha ya taaria za ukiukaji na pande zote. Marekani na washirika wake imefanya mashambulizi 12 nchini Syria na mengine 12 nchini Iraq.

Frankreich designierter Außenminister Jean-Marc Ayrault
Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa, Jean-Marc AyraultPicha: Reuters/S. Mahe

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon alisema usitishwaji mapigano Syria unatekelezwa kwa kiwango kikubwa na anataka urefushwe kupita muda uliopangwa wa wiki mbili.

Serikali ya Syria ilimshutumu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Saudi Arabia, Adel al-Jubeir, kwa kujaribu kuyavuruga makubaliano ya kusitisha mapigano kwa kusema kuna mpango mbadala. Jubeir alisema jana, bila kutoa maelezo ya kina, kuwa serikali ya Syria na mshirika wake Urusi zimekiuka makubaliano hayo na kutakuwa na mpango mbadala ikidhihirika serikali ya mjini Damascus na washirika wake hawana nia ya dhati kuutekeleza usitishaji mpigano.

Jumuiya ya NATO ina wasiwasi

Wakati haya yakiarifiwa, katibu Mkuu wa jumuiya ya kujihami ya NATO, Jens Stoltenberg, alielezea wasiwasi wake kuhusiana na ripoti za ukiukaji wa makubaliano hayo na kuzihimiza pande zote husika kuyaheshimu. Stoltenberg pia amesema NATO ina wasiwasi kuhusu Urusi kuongeza shughuli zake za kijeshi nchini Syria, ambako imekuwa ikifanya operesheni ya mashambulizi ya mabomu ya miezi mitano kumuunga mkono rais wa Syria, Bashar al Assad.

Katibu mkuu huyo alisema mashambulizi ya Urusi yamewalenga waasi ambao si wapiganaji wa jihadi, badala ya wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu, ambao wamekuwa wakishambuliwa na muungano unaoongozwa na Marekani.

Mwandishi:Josephat Charo/rtre/afpe/ape

Mhariri:Mohammed Khelef