Upinzani Syria wakutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi
15 Novemba 2011Urusi mara kwa mara imekuwa katika mstari wa mbele kupinga mataifa ya Magharibi kuiwekea vikwazo Syria kufuatia matukio ya kuwakamata waandamanaji, wanaoshinikiza umuhimu wa kuwa na mazungumzo.
Moscow imekuwa moja kati ya nchi chache zilizolaani msimamo wa jumuiya ya ya nchi za kiarabu ya kuisimamisha Syria katika Jumuiya hiyo, wakisema mpango huo tayari ulikuwa umeshapangwa na jumuiya hiyo.
Hata hivyo Waziri wa mambo ya nje Nchini Syria Wallid Muallem amesema, wako tayari kwa mazungumzo.
Mwezi uliopita rais wa Urusi Dmitry Medvedev alimtaka rais Bashar Al Assad kukubali mabadiliko ama kuachia madaraka ingawa bado hajaungana na mataifa ya magharibi yanayoshinikiza hilo. Syria ilipinga uundwaji wa baraza la kitaifa la Syria nchini uturuki mwezi uliopita wakisema hatua hiyo ni kuupinga moja kwa moja utawala wa Rais Assad.
Jumuiya ya nchi za kiarabu kwa upande wao wanajiandaa kutuma ujumbe wa watu 500 ukijumuisha watetezi wa haki za kibinaadam, waandishi wa habari na wataalamu wa jeshi kuangalia mambo yanavyokwenda na kutafuta mikakati maalum ya kulinda raia.
Huku hayo yakiarifiwa zaidi ya watu 70 waliuwawa hapo jana kufuatia mapigano makali zaidi kati ya vikosi vya usalama na waandamanaji tangu kuanza kwa wimbi la mageuzi miezi minane iliopita. Kulingana na walio shuhudia, mauaji hayo ya kinyama yalitokea katika mji wa Daraa na watu wengine 4 waliuwawa kwa kupigwa risasi katika mji wa Homs.
Umoja wa mataifa unakadiria raia zaidi ya watu 3,500 wameuwawa katika machafuko hayo nchini Syria tangu yalipoanza mjini Daraa tarehe 15 Machi mwaka huu.
Mwandishi Amina Abubakar/ AFP
Mhariri Mohammed Abdul-Rahman