1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani Syria wakubaliana kuzungumza kwa sauti moja

24 Novemba 2017

Makundi tofauti ya upinzani nchini Syria yametangaza makubaliano mapema leo ya kuutuma ujumbe wa pamoja katika mazungumzo ya Amani wiki ijayo jijini Geneva, yanayoongozwa na Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/2oAuR
Riad Treffen Syrische Opposition Mistura
Picha: Getty Images/AFP/F. Nureldine

Tangazo hilo limetolewa katika siku ya pili ya mkutano unaosimamiwa na Saudi Arabia mjini Riyadh, ambako karibu viongozi 400 wa upinzani wamekusanyika kwa ajili ya kuyaunganisha makundi yao kabla ya mazungumzo ya moja kwa moja na utawala wa Rais wa Syria Bashar al-Assad nmamo Novemba 28.

Duru kadhaa za mazungumzo yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa zimeshindwa kufikisha kikomo mgogoro wa SYRIA, ambao umewaua karibu watu 330,000 tangu mwaka wa 2011 na kuwalazimu mamilioni ya wengi kukimbia makazi yao.

Basma Qadmani ni msemaji wa upinzani Syria "Tulikubaliana na kundi la pande zilizoko hapa Riyadh na Cairo na Moscow kuhusu kuundwa kwa ujumbe wa pamoja ili kushiriki katika mazungumzo ya moja kwa moja jijini Geneva katika siku chache zijazo".

Qadmani ameongeza kuwa mikutano Zaidi itafanyika leo ili kukamilisha orodha ya majina na idadi ya wawakilishi ambao kila kundi litakuwa nao katika ujumbe wa pamoja wa watu 50.

Schweiz Genf Friedensverhandlungen Syrien - Riad Hijab
Riad Hijab alijiuzulu kama mkuu wa HNCPicha: Reuters/D. Balibouse

Wajumbe katika mkutano huo wamekuwa chini ya shinikizo kubwa kuyalegeza kiasi masharti yao makali baada ya msururu wa ushindi katika uwanja wa mapambano ambao umeupa utawala wa Assad mafanikio makubwa.

Kundi la upinzani nchini Syria lenye makao yake mjini Cairo lilikubaliana mapema jana kujiunga na makundi mengine ya upinzani ikiwemo Kamati Kuu ya Majadiliano – HNC inayoungwa mkono na Saudi Arabia – na ambalo ndilo kundi kubwa la upinzani – na Muungano wa Kitaifa wenye makao yake mjini Istanbul. Baada ya mazungumzo yaliyorefushwa ambayo yaliingia hadi usiku, kundi la upinzani nchini Syria lenye makao yake mjini Moscow pia lilionekana kuungana na ujumbe huo. Lakini kulikuwa na tofauti zilizoendelea kujitokeza baina yao.

Kundi la HNC na washirika wake wamesisitiza kuwa sharti lao la muda mrefu kuwa Assad ang'atuke madarakani kama sharti la kuwekwa awamu ya mpito ili kumaliza vita ya Syria, kitu kilichozusha wasiwasi kutoka kwa kundi la Moscow. Viongozi kadhaa waandamizi wa upinzani walisusia mkutano huo, akiwemo Jamil wa kundi la Moscow na Riad Hijab wa kundi la HNC. Hatima ya Assad imekuwa kizingiti katika duru kadhaa za mazungumzo kati ya utawala wa Syria na upinzani.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria Staffan de Mistura, alihudhuria kikao cha ufunguzi wa mazungumzo ya Riyadh siku ya Jumatano na akasema lengo la mkutano huo lilikuwa ni kuyapa msukumo mazungumzo ya Amani ya wiki ijayo.

Mazungumzo ya Riyadh yamefanywa wakati mshirika wa serikali ya Syria, Urusi ikipanga kuandaa mkutano wa kuyaleta pamoja majeshi ya Assad na makundi kadhaa ya upinzani ili kuufufua mchakato uliokwama wa Amani.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Caro Robi