Upinzani Syria wafanikiwa Munich
3 Februari 2013Urusi na Iran zimekuwa washirika wakubwa wa Rais Bashar al-Assad na makubaliano yoyote wanayoweza kufikiwa na mahasimu wa Assad yanatazamiwa kuondoa kikwazo kwa pande hizo mbili kufikia makubaliano.
Al-Khatib alikutana kwanza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, siku ya Jumamosi (tarehe 2 Februari), na inaaminika hatua hiyo ilitokana na ishara alizoonesha al-Khatib za kuwa tayari kuzungumza na serikali ya Syria.
"Urusi ina mtazamo wake mahsusi lakini kimsingi ni kuwa tunakaribisha majadiliano kuumaliza mgogoro huu na kuna mambo mengi yanayohitaji kujadiliwa," alisema al-Khatib baada ya mkutano huo.
Al-Khatib akubaliana na Iran
Baada ya mkutano wa dakika 45 na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Ali Akbar Salehi, al-Khatib aliliambia shirika la habari la Reuters: "Tumekubaliana kwamba tunalazimika kutafuta njia ya kumaliza mateso ya watu wa Syria."
Wakati kukionekana kiwango fulani cha mafanikio yaliyofikiwa Munich, vyombo vya habari vya Iran vimeripoti kwamba Mkuu wa Baraza la Usalama la nchi hiyo, Saeed Jalil, alikwenda mjini Damascus kukutana na maafisa wa serikali ya Syria na kumsaidia Assad "kusimama imara dhidi ya njama zinazochochewa na kiburi cha ulimwengu" - kauli inayoelekezwa Marekani na mataifa ya Magharibi.
Al-Khatib alikutana pia na Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden, na mjumbe maalum wa kimataifa kwa Syria, Lakhdar Brahimi.
Kiongozi mwengine wa upinzani wa Syria, Hassan Bali, ambaye yuko mjini Munich kama mwangalizi wa kujitegemea, aliuita mkutano wa al-Khatib na Biden kama "ishara kubwa kutoka kwa Wamarekani" kwamba wanaongeza msaada wao kwa waasi wanaopigana kumuangusha Assad.
Biden anasema alimtolea wito al-Khatib kuwatenga wapiganaji wenye itikadi kali za kidini na ´pia kuzikaribisha jamii nyengine kwenye upinzani, wakiwemo Wakristo, Wakurdi na hata watu wa kabila la Assad la Alawi.
Dhamira ya upinzani
Lengo la kiongozi huyo wa Muungano wa Baraza la Kitaifa la Syria kwenye mikutano hiyo lilikuwa ni kujadiliana namna ya kupata njia ya kuuondoa utawala "bila ya kuendelea kumwaga damu na kupoteza maisha."
Urusi imewahi kuzuia maazimio matatu ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yaliyodhamiria kumuondoa Assad madarakani au kumshinikiza kuzuia vita vya wenyewe kwa wenyewe, ambavyo hadi sasa vimeshagharimu maisha ya zaidi ya watu 60,000. Lakini serikali ya Urusi imejaribu pia kujitena na Assad ikisema kwamba haijaribu kumlinda na kwamba haitampa hifadhi.
Kauli ya Waziri Mkuu wa Urusi, Dmitry Medvedev, wiki hii kwamba fursa za Assad kubakia madarakani zinazidi kupungua, ilichukuliwa kama ishara ya kubadilika kwa sera ya serikali ya Urusi kuelekea Syria.
"Mazungumzo juu ya Syria yanazidi kushika kasi na Wairani sasa wameingizwa. Wacha tuone yatakavyomaliza," kilisema chanzo kimoja cha kidiplomasia.
Mgawanyiko kwenye upinzani
Mapema wiki hii, al-Khatib alihatarisha madaraka yake ndani ya vuguvugu la upinzani pale alipodaiwa kukiuka taratibu kwa kusema kwamba alikuwa tayari kukutana na maafisa wa serikali ya Syria kujadiliana kipindi cha mpito ikiwa wafungwa wa kisiasa wataachiliwa huru.
Kamati kuu ya kisiasa ya muungano huo wa upinzani yenye wajumbe 12 ilimwambia al-Khatib kwamba asikubali mapendekezo yoyote yatakayotolewa Munich bila ya kwanza kushauriana nao, huku chanzo kimoja kutoka upinzani kikisema kwamba hatua hiyo ya al-Khatib inaweza kuwavunja moyo wapambanaji.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayemaliza muda wake, Hillary Clinton, aliupongeza utayarifu wa al-Khatib kukutana na wajumbe wa Assad nje ya Syria, akisema "sio tu ni shujaa bali pia mtu madhubuti." Clinton pia alionyesha wasiwasi wake kwamba kwa siku za hivi karibuni, Iran imeongeza msaada wake wa kijeshi kwa Assad.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Grace Patricia Kabogo