1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Senegal wapinga uwezekano wa Rais Sall kuwania tena Urais

13 Mei 2023

Mamia ya wafuasi wa upinzani nchini Senegal waliandama jana Ijumaa kupinga uwezekano wa kuwepo jaribio la rais wa nchi hiyo Macky Sall kuwania muhula wa tatu madarakani.

https://p.dw.com/p/4RIaU
Senegalese President Macky Sall
Picha: Presidency of Senegal / Handout/AA/picture alliance

Maandamano hayo ni mwendelezo wa mikusanyiko ya vurugu inayoshuhudiwa nchini Senegal kupaza sauti juu ya masuala kadhaa ikiwemo wasiwasi wa upinzani kuwa rais Sall huenda anapanga kugombea kwa muhula wa tatu.

Sall, mwenye umri wa miaka 61 aliingia madarakani mwaka 2012 na kushinda muhula wa pili mwaka 2019. Hata hivyo katiba mpya ya Senegal iliyopitishwa mwaka 2016 inaweka ukomo kwa rais kuongoza kwa mihula miwili ya miaka mitano.

Ingawa Sall hajathibitisha mipango ya kugombea tena, hivi karibuni aliliambia gazeti moja la Ufaransa kwamba anaweza kuwania muhula mwingine kwa sababu muhula wake wa kwanza wa uongozi chini ya katiba mpya ulianza baada ya kuchaguliwa tena mwaka 2019.