Upinzani nchini Mali waitisha maandamano zaidi
20 Julai 2020Rais Ibrahim Boubakar Keita ambaye amesalia na miaka mitatu tu katika muhula wake wa mwisho, anakabiliwa na shinikizo za kutaka ajiuzulu tangu mwanzoni mwa mwezi Juni.
Umaarufu wake umeshuka kutokana na madai ya ufisadi yanayoizonga serikali yake huku mzozo wa wapiganaji wa Kiislamu wenye itikadi kali ukiendelea kuitia doa serikali yake.
Wito wa kumtaka rais huyo ajiuzulu umeongezeka baada ya maandamano ya hivi karibuni kujibiwa vikali na vikosi vya usalama, na kusababisha kifo cha kiasi ya watu 12.
Maandamano hayo yalisitishwa kwa muda wakati wa mazungumzo na wapatanishi 15 kutoka jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya Afrika Magharibi Ecowas, lakini muungano wa upinzani unaofahamikama kama Juni 5 umeitisha tena maandamano baada ya kuukataa mpango wa Ecowas.