Upinzani Kongo wapinga kuletwa kwa wanajeshi wa SADC
11 Mei 2023Kauli ya upinzani wa Lamuka inatokea muda mfupi baada ya SADC kuamua kupeleka wanajeshi wake mashariki mwa DRC kurejesha amani na usalama huko.
Katika taarifa kwa wanahabari, upinzani huo wa kisiasa unasikitikia namna ambavyo ardhi ya Kongo inadhulumiwa na unapendekeza kwamba jeshi la Congo lipewe thamani kwa kupewa vifaa mhimu na mshahara mzuri kwa askari ili wapambane na hali ya ukosefu wa usalama mashariki ya Kongo.
Hata hivyo, maelezo kadhaa bado yanasalia kitendawili, kama vile tarehe na maeneo ya kupelekwa kwa wanajeshi wa SADC wanaotarajiwa Kongo.
Pia hadi sasa haijajulikana idadi ya wanajeshi ambao wataunda kikosi hicho au pia idadi kamili ya nchi zinazochangia kuleta askari wake ndani ya kikosi hicho.
Lakini pia maswali kadhaa hayajapata jibu ikiwa kwa mfano Afrika Kusini itashiriki katika kikosi cha SADC ijapokuwa askari wake wako ndani ya tume ya amani ya umoja wa mataifa nchini Kongo MONUSCO, au Angola ambayo hivi karibuni imeahidi kutuma wanajeshi 500 katika eneo la mashariki mwa Kongo ili kulinda maeneo ambayo wapiganaji wa M23 watakuwa wamepangwa.
Upinzani wa Lamuka unaandaa maandamano Jumamosi ijayo mjini Kinshasa ili kuunga mkono jeshi la Kongo FARDC na kutaka majeshi ya Rwanda kuondoka nchini humo.