1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani DRC walalamikia hitilafu katika uchaguzi

Daniel Gakuba
31 Desemba 2018

Kambi muhimu ya upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imedai uchaguzi wa jana Jumapili ulikumbwa na changamoto nyingi, zikiwemo kukwama kwa kompyuta za kupigia kura, na mvua kubwa katika maeneo mengi na vurugu.

https://p.dw.com/p/3Ao87
Kongo hält mit zwei Jahren Verspätung historische Wahlen ab
Picha: Reuters/K. Katombe

Zoezi la upigaji kura katika uchaguzi wa kumtafuta mrithi wa Rais Joseph Kabila liliendelea hadi jioni katika baadhi ya vitongoji vya jiji la Kinshasa Jumapili, ambako vituo vilichelewa kufunguliwa kutokana na kukosekana kwa madaftari yenye orodha ya wapiga kura.

Mkutano wa maaskofu Katoliki wenye ushawishi DRC umesema mashine ya kupigia kura ambazo tangu mwanzo zililalamikiwa na upinzani zilikwama katika vituo 544 kati ya 12,300 walivyovikagua katika maeneo mbali mbali ya nchi.

Mmoja wa wagombea wanaopewa nafasi ya kushinda urais, Felix Tshisekedi amesema inaovyoonekana Kabila anaweza kuendelea kubaki madarakani, ikiwa uchaguzi utafutwa kutokana na hitilafu zilizobainika.

''Mambo yamevurugika kiasi kwamba tunashuku pengine ni vurugu za kupangwa, kwa makusudi ya kuipa Mahakama ya Katiba kisingizio cha kuufuta uchaguzi huu kesho.'' Amelalamika Tshisekedi.

Kura zaanza kuhesabiwa

Wahlen im Kongo
Rais Joseph Kabila ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 18Picha: picture-alliance/AP/J. Delay

Katika baadhi ya maeneo ya nchi, maafisa wa uchaguzi walianza kuhesabu kura kwa kutumia mwanga wa kurunzi, huku wakiziandika kwenye vibao vya madarasani. Matokeo ya awali yanatarajiwa kutolewa katika muda wa siku chache.

Ingawa kwa sehemu kubwa uchaguzi ulifanyika katika mazingira yenye utulivu kwenye maeneo mengi ya taifa hilo lenye eneo kubwa, kulikuwepo baadhi ya visa vya fujo.

Katika kituo kimoja cha kupigia kura katika jimbo la Kivu ya Kusini Mashariki mwa nchi, polisi alimpiga risasi na kumuuwa kijana mmoja baada ya kuzozana kuhusu madai ya ulaghai katika zoezi la upigaji kura.

Umati wa watu waliokuwepo walilipiza kisasi kwa kumpiga polisi huyo hadi kufa. Haya yamethibitishwa na mashahidi na wanasiasa waliokuwepo mahali hapo. Katika ghasia hizo, afisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (CENI) pia aliuawa.

Tukio la kihistoria

Wahlen im Kongo
Uchaguzi ni tukio la nadra DRCPicha: Reuters/B. Ratner

Uchaguzi ni tukio la nadra nchini DR Congo, ambayo tangu ulipopata uhuru kutoka ukoloni wa kibelgiji, imekumbwa na utawala wa kiimla, mauaji ya kisiasa, mapinduzi ya kijeshi na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Ikiwa Joseph Kabila ambaye amekuwa madarakani tangu kuuawa kwa baba yake mwaka 2001 ataondoka madarakani baada ya uchaguzi huu, itakuwa mara ya kwanza kwa nchi hiyo kubadilishana madaraka kwa njia ya amani.

Lakini ikiwa matokeo ya uchaguzi huo yataleta mzozo, hali ya usalama inaweza kuzorota haraka, hususan katika eneo la Mashariki kwenye mpaka baina ya nchi hiyo na Rwanda, Uganda na Burundi, ambako kuna makundi kadhaa yenye silaha.

Uchunguzi wa maoni kuelekea siku ya uchaguzi ulikuwa ukionyesha wagombea wa upinzani wakiongoza.

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre, ape

Mhariri: Iddi Ssessanga