Uongozi wa Barack Obama kwa mtazamo wa picha
Huku uongozi wa Barack Obama ukifikia kikomo, DW inaangazia wakati wake katika ikulu. Kutoka mabadiliko ya huduma za afya hadi katika ikulu inayopendeza, ufuatao ni mkusanyiko wa nyakati muhimu.
'Hatimaye'
Siku aliyoapishwa Obama kuwa rais wa 44 wa Marekani ilikuwa hafla ya kihistoria nchini humo. Tarehe 20 mwezi Januari 2009, zaidi ya miaka 230 iliyopita baada ya kuundwa kwake, nchi hiyo ilipata rais wake wa kwanza Mwafrika. "Hatimaye," msanii Beyonce aliimba wakati wa dhifa ya kwanza rasmi kwa rais huyo huku akicheza muziki huo na mkewe kwa mara ya kwanza madarakani.
Nchi iliyoko matatani
Obama alianza muhula wake wa kwanza madarakani huku kukiwa na mzozo mkubwa wa kiuchumi tangu kutokea kwa mdororo mkubwa wa kiuchumi nchini Marekani. Siku chache baada ya kuapishwa, Obama alitia saini muswada wa kuchochea uchumi kuwa sheria ikiwa ni pamoja na kupunguzwa kwa viwango vya riba na uwekezaji wa miundombinu yenye thamani ya Dola milioni 800.
Bima ya afya kwa Wamarekani milioni 20
Mnamo mwezi Machi, 2010, Obama alitimiza moja ya ahadi zake kuu za kampeini. Alitia saini sheria ya huduma nafuu za afya. Sheria ya "Obamacare" iliyokabiliwa na utata mwingi ikiwa ni pamoja na hatua za kisheria huku mrithi wa Obama, Donald Trump, akiapa kufutilia mbali sheria hiyo aliyoitaja kuwa mzigo kwa Wamarekani.
Tuzo ya amani ya Nobel licha ya vita na mashambulizi ya ndege zisizokuwa na rubani.
Baada ya chini ya mwaka mmoja katika urais, kamati ya tuzo ya Nobel ilimtunuku Obama tuzo ya amani ya Nobel katika juhudi zake za kuimarisha diplomasia ya kimataifa na ushirikiano baina ya watu." Shtuma zilikithiri kuhusiana na kutolewa kwa tuzo hiyo kwa rais aliyekuwa akitekeleza vita viwili na mpango wa mashambulizi ya ndege zisizokuwa na rubani yaliyosababisha vifo vya mamia ya watu.
Kifo cha adui wa jadi na kuzaliwa kwa wengine wapya
Baada ya muongo wa kusakwa, Osama Bin Laden, kiongozi wa al Qaeda aliuawa na wanajeshi wa Marekani nchini Pakistan mwezi Mei, 2011. Obama alitangaza haya kwa ulimwengu mzima kupitia hotuba ya runinga. Lakini kifo cha bin Laden hakikumaliza kero la ugaidi katika uongozi wake. Mnamo mwaka 2014, Marekani ilianzisha mashambulizi ya angani dhidi kundi la wanamgambo wanaojiita 'Dola la Kiislamu.'
Kutoka mwanzo mpya kufikia mvutano
Obama alianza uongozi wake kwa ahadi ya kuanzisha upya uhusiano wa Marekani na Urusi, hata kumpeleka aliyekuwa rais Dmitry Medvedev kupata chakula mwaka 2010. Lakini kutekwa kwa eneo la Crimea mwaka 2014, Urusi kumuunga mkono Rais wa Syria, Bashar al-Assad na shutuma dhidi ya Urusi kwa kuingilia uchaguzi wa Marekani, kulisababisha uhasama kati ya mataifa hayo mawili.
Agizo la rais kuhusu uhamiaji
Juni, 2012, Obama alitia saini agizo la rais la kuruhusu wahamiaji wenye umri mdogo ambao hawajasajiliwa kusoma nchini Marekani ama wale waliohudumu katika jeshi kuishi Marekani. Miaka minne baadaye, mahakama ya juu ilipinga agizo hilo kwa kura 4 kati ya 4. Akikabiliwa na bunge la wanachama wengi wa Republican, Obama mara nyingi alitumia maagizo ya rais kushinikiza agenda zake za sera.
Miaka minne zaidi
Novemba 2012, Obama alipata ushindi mwingine wa urais - japo alishinda kwa kura chache dhidi ya Mitt Romney kuliko alivyoshinda dhidi ya John McCain mwaka 2008. Katika hotuba yake baada ya kuchaguliwa mara ya pili, Obama aliweka malengo ya uongozi wake ikiwa ni pamoja na kulinda haki za mashoga na wasagaji, kulinda mazingira, marekebisho katika uhamiaji na udhibiti wa bunduki.
Rais wa rangi nyingi
Obama alikuwa rais wa kwanza wa Marekani kuidhinisha ndoa kati ya watu wa jinsia moja. Huku awali akiwa ameunga mkono mashirika ya kijamii, alizungmza kwa mara ya kwanza kupendelea ndoa za jinsia moja wakati wa kampeini yake ya mwaka 2012. Wakati mahakama ya juu ilipoamua kuwa ndoa hiyo zinapaswa kuwa halali mwezi Juni, 2015, Ikulu ya rais iliwashwa rangi mbali mbali kuunga mkono hatua hiyo.
Karibu Cuba
Obama aliangazia upya uhusiano wa Marekani na Cuba iliyoiwekea vikwazo vingi. Alipozuru kisiwa hicho Machi, 2016, alikuwa rais wa kwanza wa Marekani kuzuru nchi hiyo katika muda wa miaka 88. Mwishoni mwa mwaka 2014, Rais wa Cuba, Raul Castro na Obama walitangaza kuwa wataanzisha upya uhusiano wa kidiplomasia. Obama aliondoa kikwazo cha usafiri na kufungua ubalozi wa Marekani mjini Havana.
Ang'ara zaidi
Obama mara kwa mara aling'ara kuliko wachekeshaji waliomualika katika vipindi vyao vya runinga, kama pale alipoimba taarifa ya habari na mtangazaji Jimmy Fallon au alipokuwa mgeni katika kipindi cha "Between Two Ferns" na Zach Galifianakis. Obama mara nyingi alionyesha ueledi wake wa kuzungumza na kutoa vichekesho huku hotuba zake zikiwaacha wengi na vicheko.
Raia wa kwanza wa Amerika Kusini katika mahakama ya juu
Obama aliwateuwa wanawake wawili kuhudumu katika mahakama ya juu ya Marekani - Elena Kagan na Sonia Sotomayor. Pichani katikati ni jaji wa kwanza wa Amerika Kusini kuhudumu katika mahakama hiyo ya juu zaidi Marekani. Hii ilisababisha idadi ya majaji wanawake kufikia watatu kati ya tisa.
Bado ni hatua katika kuifikia Marekani isiyokuwa na ubaguzi wa rangi
Uchaguzi wa Obama mara nyingi ulitajwa kuwa mwisho wa ubaguzi wa rangi Marekani, lakini kusita kuzungumzia suala hilo mara ya kwanza kuliwavunja wengi moyo. Mnamo Machi, 2015, alizungumza huko Selma, Alabama, akitaja ufanisi uliopatikana miaka 50 ya awali wakati polisi walipowapiga waandamanaji, lakini akakiri kuwa msukumo wa haki sawa haujafikia kikomo.
Gereza la Guantanamo Bay bado liko wazi
Licha ya agizo alilotia saini siku ya pili mdarakani, Obama alishindwa kutimiza ahadi ya kuifunga jela ya kijeshi ya Guantanamo Bay, Cuba. Eneo la mateso na kizuizi bila kufunguliwa mashtaka kwa zaidi ya muongo mmoja, Obama alisema Marekani ilisaliti maadili yake muhimu huko Guantanamo. Katika siku zake za mwisho za urais, wafungwa wengine waliachiliwa huru lakini wengi bado wako kizuizini.