1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uongozi mpya wa walinzi wa mazingira magazetini

9 Oktoba 2013

Walinzi wa mazingira kujipatia uongozi mpya,kushindwa mradi wa nishati mbadala,na lawama anazotupiwa askofu mkuu wa Limburg ndizo mada zilizochambuliwa zaidi na wahariri wa magazeti ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/19wih
Kerstin Andreae wa walinzi wa mazingiraPicha: picture alliance / Eventpress

Walinzi wa mazingira kujipatia uongozi mpya,kushindwa mradi wa nishati mbadala,sheria ya kuharibu mimba Uingereza na lawama anazotupiwa askofu mkuu wa Limburg ndizo mada zilizochambuliwa zaidi na wahariri wa magazeti ya Ujerumani.

Tuanzie lakini na uongozi mpya wa chama cha walinzi wa mazingira die Grüne.Gazeti la "Badische Neueste Allgemeine" linaandika:"Uongozi mpya wa walinzi wa mazingira bado si timamu.Zaidi ni kwamba walinzi wa mazingira wanaelemea zaidi mrengo wa shoto,muda mfupi kabla ya mazungumzo,ya kupima uwezekano wa kuunda serikali kuu ya muungano pamoja na Christian Democratic Union-CDU/na Christian Social Union-CSU na kuiacha tupu nafasi ya mrengo wa kati,baada ya kushindwa kuwakilishwa bungeni waliberali wa FDP.Kwa kumchagua Kerstin Andreae kuwa mkuu wa kundi la wabunge wa die Grüne,walinzi wa mazingira wamepanua ujuzi wao na kufungua njia ya kuleta uwiano kati ya mazingira na uchumi.

Windkraft in Schleswig-Holstein
Nishati inayotokana na nguvu za upepo katika jimbo la Schleswig-HolsteinPicha: DW/G.Rueter

Mradi mkubwa wa nishati mbadala huenda ukafeli

Gazeti la "Donaukurier" linaandika kuhusu mageuzi katika sera ya nishati:"Wengi wa wanasiasa wanatambua kwamba mradi uliokuwa ukipigiwa upatu unakurubia kufeli.Lakini hakuna anaesubutu kutamka hilo hadharani.Mada ya mageuzi katika sekta ya nishati ilikuwa ikitukuzwa sana miaka iliyopita humu nchini.Ilikuwa miko kuiwekea mada hiyo suala la kuuliza.Lakini ukweli haufichiki kwa muda mrefu.Wakati umewadia,watu kuzungumzia kinaga ubaga kama mradi huo haujafeli moja kwa moja.

Deutschland Kirchen Kaaba Bischofssitz in Limburg
Kanisa la nyumba ya askofu mkuu wa LimburgPicha: picture-alliance/dpa

Kashfa katika ujenzi wa nyumba ya askofu mkuu wa Limburg

Mada nyengine iliyogonga vichwa vya habari inahusiana na diosisi ya Limburg.Baada ya gharama za ujenzi wa nyumba ya askofu mkuu wa Limburg kukithiri,sauti zinaongezeka kumtaka askofu mkuu ajiuzulu.Gazeti la Hessische Niedersächsische Allgemeine" linahisi gharama zilizopindukia si jambo jipya:" Ikiwa diosisis ya Limburg itahitaji siku za mbele kumpata askofu mkuu mwengine,sabababu isiwe gharama zilizokithiri za ujenzi wa makaazi ya askofu mkuu kutoka Euro milioni tatu na kufikia Euro milioni 31.Makosa katika kupiga hesabu kila kwa mara yanatokea nchini Ujerumani:kwa mfano mjini Hamburg,Berlin na Stuttgart.Hesabu mbaya zinabainisha makosa yanayotokea katika tangazo na pia katika uongozi.Limburg hali ilikuwa hivyo hivyo.Lakini Mtaji mkubwa wa askofu mkuu sio Euro milioni tatu au 30,bali imani.Kwamba imani hiyo sasa haipo tena hilo ni pigo kubwa kwa askofu mkuu wa Limburg,Franz-Peter Tebartz-van Elst.

Sheria ya kuharibu mimba Uingereza

Ripoti yetu ya mwisho magazeti kwa leo inatufikisha Uingereza ambako mtindo wa kuharibu mimba unaruhusiwa kisheria.Gazeti la "Bild" linaandika:"Nchini Uingereza ni halali mtu kuharibu mimba,ikiwa wazee wanaona mtoto atakaezaliwa si wa jinsia wanayoitaka.Hakuna sheria inayopiga marufuku jambo hilo.Vipi jambo kama hilo likawezekana.Mfumo wa sheria sio tu hauthamini utu na ni wa enzi za kale bali pia unatoa ishara mbaya kwa nchi zinazofuata tamaduni nyengine.Hata India,kuharibu mimba kwasababu ya jinsia ni marufuku.Licha ya hayo maelfu ya watoto wachanga wanazamishwa baharini kwasababu wamezaliwa na jinsia ya kike.Watafikiria nini wanaofanya hivyo nchini humo wakisikia katikla nchi ya Umoja wa ulaya watu wanaruhusiwa kuharibu mimba ikiwa mtoto atakaezaliwa ni mwanamke?Sheria hiyo ya aibu lazma ibatilishwe tena haraka.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri. Mohammed Abdul-Rahman