1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa watuhumiwa

10 Juni 2015

Ripoti mpya iliyofichuliwa la shirika la habari, Associated Press, inaonyesha kuwa matukio ya unyanyasaji wa kingono bado hayaripotiwi katika operesheni za wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/1FeRH
Brasilianische Blauhelme in Haiti
Picha: AP

Hii ni baada ya kugundulika kuwa wanajeshi wa kulinda amani walihusika katika kile kinachoitwa “ngono ya makubaliano” na zaidi ya wanawake 225 wa Haiti ambao walisema walihitaji kufanya hivyo ili kupewa vitu kama chakula na matibabu.

Rasimu ya Ripoti ya Ofisi ya Huduma za Usimamizi wa Ndani inaangalia namna ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, ambao una zaidi ya wanajeshi 125,000 katika baadhi ya maeneo yenye migogoro mikubwa duniani, unavyoshughulikia tatizo hili lililokothiri la unyanyasaji kingono.

Ripoti hiyo, inayotarajiwa kutolewa mwezi huu, inasema mabadiliko makubwa hayajafanyika, mwongo mmoja baada ya ripoti ya Umoja wa Mataifa kuliangazia suala hilo kwa mara ya kwanza.

Miongoni mwa matokeo ya uchunguzi huo: thuluthi moja ya visa vinavyodaiwa vya unyanyasaji kingono vinawahusisha watoto wa chini ya miaka 18. Msaada kwa waathiriwa unakosekana kwa kiwango kikubwa. Na uchunguzi wa wastani unaofanywa na ofisi ya usimamizi, ambayo huyapa kipau mbele matendo yanayowahusisha watoto au ubakaji, huchukua zaidi ya mwaka mmoja.

UN Blauhelme Geschichte
Mwanajeshi wa kulinda amani nchini HaitiPicha: AP

Ripoti hiyo inasema, mwaka mmoja uliopita, waliwahoji watu 231 nchini Hairi waliosema kuwa walikuwa na mahusiano ya kingono kwa mapatano na wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa. Wanawake wa vijijini walifanya hivyo kwa ajili ya njaa, ukosefu wa makaazi, vifaa vya kuwatunza watoto, matibabu na vitu vya nyumbani. Nao wanawake wa mijini walipewa viatu vya thamani kubwa, simu za mkononi, laptop na marashi pamoja na fedha.

Kwa kipindi kizima cha mwaka uliopita, idadi ya jumla ya matukio ya madai ya unyanyasaji kingono dhidi ya wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa ilikuwa 51, ikiwa ni chini kutoka 66 mwaka uliotangulia, kwa mujibu wa ripoti ya karibuni ya katibu mkuu kuhusu suala hilo inayotolewa kila mwaka.

Ujumbe wa kulinda amani uliidhinishwa kwa mara ya kwanza nchini Haiti, katika mwaka wa 2004 na kufikia mwishoni mwa Machi, ulikuwa na karibu wanajeshi 7,000. Haiti ni mojawapo ya nchi ambazo wanajeshi wa kulinda amani wamehusishwa na madai mengi ya unyanyasaji kingono katika miaka ya karibuni, pamoja na wale walioko Congo, Liberia na Sudan Kusini, na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Umoja wa Mataifa hauna jeshi lake, na hutegemea majeshi yanayotolewa na mataifa wanachama. Mataifa hayo yana wajibu wa kuchunguza maai ya ukosefu wa nidhamu wa majeshi yao, ijapokuwa Umoja wa Mataifa unaweza kuingilia kati ikiwa hatua haichukuliwi.

Katika kujibu matokeo ya uchunguzi huo, ambayo yamejumuishwa kwenye rasimu hiyo, mkuu wa operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa Herve Ladsous na mkuu wa idara ya operesheni Atul Khare wanasema kuwa wakati idadi ya wanajeshi imepungua kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha mwongo mmoja uliopita, idadi ya madai ya matukio ya unyanyasaji kingono imepungua.

Mwandishi: Bruce Amani/AP
Mhariri: Mohammed Khelef