1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Unyakuzi wa ardhi wajadiliwa Rio + 20

21 Juni 2012

Mkutano wa kimataifa wa mazingira wa Rio + 20 unaendelea mjini Rio de Janeiro, Brazil. Miongoni mwa mada zinazozungumziwa kwa kina na wawakilishi wa nchi za Afrika na mashirika yasiyo ya kiserikali ni unyakuzi wa ardhi.

https://p.dw.com/p/15JC3
Shamba nchini Senegal
Shamba nchini SenegalPicha: picture alliance/Godong

Suala kuu la malalamiko ni kwamba mashirika makubwa kutoka nje yanaingia Afrika na kujinyakulia maelfu ya hekta za ardhi. Kuanzia mashariki hadi magharibi mwa bara la Afrika, suala hilo limekuwa tatizo kubwa sana. Kiongozi wa chama cha wakulima wanawake wa Sierra Leone, Bi Sarah Rogers, anaeleza kuwa unyakuzi wa ardhi umekuwa changamoto kubwa zaidi inayowakumba wakulima nchini mwake. "Asilimia 55 ya wanawake waishio vijijini ni wakulima. Wanategemea mashamba yao ya mboga. Watawezaje kujipatia mashamba mengi zaidi? Hizi ndizo changamoto tunazokabiliana nazo."

Tatizo la mgogoro wa ardhi linaweza kuongezeka katika siku za usoni. Ibrahim Ouadragogo kutoka Burkina Faso amejiunga na shirika lisilo la kiserikali kwa ajili ya kupigania hatua ya kuwarejeshea raia wa nchi yake mashamba yao. "Kwa kweli hali ni tete. Tunapaswa kukumbuka kwamba wapo watu walionyang'anywa mashamba yao kinyume na sheria. Panaweza kutokea maandamano na vurugu ambazo zinaweza kusababisha hata vifo vya watu."

Mashamba ya miwa Sierra Leone
Mashamba ya miwa Sierra LeonePicha: DW

Umoja wa Mataifa wataka mazungumzo yafanyike

Hii ndio sababu iliyowafanya wawakilishi wa mashirika yasiyo ya kiserikali kufikisha matakwa yao kwa washiriki wa mkutano wa mazingira wa Rio + 20 unaoendelea hivi sasa. Idi Ba, ambaye ni mwanachama wa shirika linalohusika na ulinzi wa mazingira katika nchi zinazoendelea, liitwalo Environment and Development Action, anafafanua: "Uporaji wa mashamba lazima ukomeshwe. Wakulima walionyang'anywa mashamba yao lazima warejeshewe mali yao. Lazima wapewe haki zao. Ni lazima tuseme hapana kwa unyakuzi wa ardhi na ndiyo kwa mabadiliko ya sera za ardhi zinazojumuisha wahusika wote."


Umoja wa Mataifa tayari imeshatoa mapendekezo kuhusu namna ya kulitatua tatizo la uporaji wa ardhi. Umoja huo unataka wadau wote wakae katika meza moja na kufanya mazungumzo. Lakini Idi Ba anaeleza kuwa Waafrika hawawezi kukubaliana na mapendekezo yanayotolewa katika mazungumzo. Kunachotakiwa ni usitishaji wa unyakuzi wa ardhi utakaofuata utaratibu fulani.

Umoja wa Mataifa wataka mazungumzo yafanyike
Umoja wa Mataifa wataka mazungumzo yafanyike

Wawakilishi wa jumuiya za kirai wanataka kuongeza shinikizo dhidi ya serikali za mataifa mbali mbali katika mkutano unaoendelea Rio de Janeiro. Wao wanasema kuwa unyakuzi wa ardhi ndio chanzo cha majanga ya njaa na migogoro katika bara la Afrika.


Mwandishi: Noël Kokou Tadegnon
Tafsiri: Elizabeth Shoo
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman