UNICEF yatoa ripoti ya udhalilishaji kwa watoto
5 Septemba 2014Katika utafiti uliofanywa juu ya unyanyasaji dhidi ya watoto, shirika hilo linaloshughulikia masuala ya watoto UNICEF limesema asilimia 20 ya waathiriwa wa mauaji ni watoto walio chini ya miaka hiyo 20.
Mauaji ni sababu kubwa ya vifo miongoni mwa watoto wa kiume na vijana wa kiume walio na miaka 10 hadi 19 katika mataifa ya Amerika ya Kusini, yakiwemo mataifa kama Venezuela, Colombia, Panama na Brazil.
Aidha shirika linaloangalia masuala ya watoto UNICEF limesema utafiti huo ni mkubwa kabisa kuwahi kufanywa juu ya unyanyasaji dhidi ya watoto, uliokusanya data kutoka nchi 190. "Hizi ni habari za uhakika zinazotia wasiwasi sana, hakuna serikali au mzazi anayetaka kuviona visa hivi," alisema mkurugenzi wa UNICEF Anthony Lake.
Visa vingine vya udhalilishaji kwa watoto ni pamoja na uonevu, ambao kwa kawaida unawaathiri zaidi ya moja kati ya watoto watatu wa shule walio kati ya miaka 13 hadi 15 duniani. Na katika visa vya kuadhibiwa ripoti hiyo ya UNICEF imegundua kwamba asilimia 17 ya vijana katika mataifa 58 wanapigwa, ikiwemo kuumizwa kichwani, masikio au uso na hali hii inasemekana kufanyika mara kwa mara.
UNICEF imesema kiwango cha unyanyasaji ni kikubwa zaidi kwa asilimia 70 au zaidi katika mataifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Guinea, Uganda Tanzania na Zimbabwe kiwango cha unyanyasaji kimesemakana kufikia asilimia 50 huku nchini Uswisi kulingana na utafiti uliofanywa mwaka 2009, ukionesha asilimia 22 ya wasichana na asilimia 8 ya wavulana walio na miaka 15 hadi 17 wakipa wamepitia aina moja ya unyanyasaji.
Mikakati ya kupamabana na Unyanyasaji dhidi ya watoto yatolewa
Nigeria pia imetajwa katika ripoti hiyo haswa katika kisa cha kuwateka nyara zaidi ya watoto 200 katika eneo la Chibok kuwa moja pia ya aina ya nyanyasaji dhidi ya watoto.
Kwa upande wake mkuu wa ulinzi wa watoto katika shirika la UNICEF Susan Bissell amesema hili ni tatizo la dunia, hakuna mtu aliyesalimika kutoka nchi tajiri, nchi masikini, Kaskazini, Kusini Mashariki hadi Magharibi.
"Cha kusikitisha ni kwamba, tunaona kitu kinachotuunganisha na ubinaadamu kwa sasa hivi ni uwezo wetu wa kuwanyanyasa watoto wetu," alisema Bi Bissel.
Mkuu huyo wa ulinzi wa watoto katika shirika la UNICEF ameongezea kuwa sio lazima hali iwe vile ilivyo kwa sasa, kumekuwa na mifano mingi iliofanana ya kusitisha unyanyasaji na hilo ndilo linalopaswa kuigwa huku akitoa wito kwa watu wote kusimama imara na kuwa sauti za watoto kwa kuwalinda.
Hata hivyo ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa imependekeza njia sita za kukabiliana na unyanyasaji dhidi ya watoto, ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wazazi kuwapa watoto mafunzo juu ya stadi za maisha, kubadilisha tabia, kuongeza makali katika sheria na mahakama dhidi ya wanaopatikana na kosa la unyanyasaji wa watoto, kuimarishwa kwa huduma na mifumo inayoshughulikia masuala ya kijamii na uhalifu na hata kuhamasisha umma juu ya madhara ya unyanyasaji kwa binaadamu na kiuchumi ili kubadilisha mitazamo ya watu juu ya suala hilo.
Mwandishi: Amina Abubakar/Reauters/afp
Mhariri:Josephat Charo