UNICEF: Watoto wa Jamhuri ya Afrika ya kati wanateseka
30 Novemba 2018Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia watoto UNICEF limeonya kuwa miaka mitano baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kuzuka katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, maisha yamekuwa magumu mno kwa watoto wa nchi hiyo.
Watoto milioni 1.5 ambao ni sawa na theluthi mbili ya wasichana na wavulana wanahitaji misaada ya kibinadamu katika taifa hilo linalokumbwa na mizozo lenye idadi ya wtau milioni tano.
UNICEF inakadiria ifikapo mwaka ujao, zaidi ya watoto 43,000 wa chini ya umri wa miaka mitano wanakabiliwa na kitisho kikubwa cha kufariki dunia kutokana uatapia mlo mbaya.
Mwakilishi wa shirika hilo katika Jamhuri ya Afrika ya Kati Christine Muhigana amesema mzozo huo unafanyika katika mojawapo ya mataifa masikini zaidi duniani na hali ya watoto ni ya kutia wasiwasi mkubwa.
Mtoto mmoja kati ya wanne aidha hana makaazi nchini humo au ni mkimbizi, huku maelfu wakilazimishwa kujiunga na makundi ya waasi au wakinyanyaswa kingono.