1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNICEF: Watoto milioni 13 Afrika hawakupewa chanjo

Sylvia Mwehozi
20 Aprili 2023

Ripoti mpya iliyotolewa wiki hii na shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto UNICEF inasema karibu watu milioni 13 hawakupata chanjo moja au zaidi barani Afrika kati ya mwaka 2019 na 2021 kwasababu ya Covid-19.

https://p.dw.com/p/4QMpn
Ethiopia| chanjo
Watoto wakipata chanjo mkoani Tigray EthiopiaPicha: Million Hailesilassie/DW

Ripoti hiyo mpya imebainisha kwamba athari za janga la Covid-19 kulichangia watoto karibu milioni 13 kukosa kupatiwa chanjo na hivyo kuliacha bara hilo katika hatari ya milipuko zaidi ya magonjwa na kukabiliwa na "mgogoro wa kuishi kwa mtoto".

UNICEF imeutaja mgogoro huo wa kimataifa katika utoaji chanjo kwa watoto kwa kipindi cha miaka mitatu kuwa mgogoro mbaya zaidi wa chanjo za utotoni ndani ya miaka 30. Afrika ni eneo ambalo lina idadi kubwa ya watoto ambao hawajachanjwa au kupatiwa chanjo pungufu. Kulingana na UNICEF, watoto milioni 12.7 barani afrika hawakupata chanjo moja au zaidi na wengine milioni 8.7 hawakupata hata dozi ya kwanza ya chanjo yoyote katika kipindi hicho.

Ethiopia| Chanjo
Watoto wakipatiwa chanjo EthiopiaPicha: Million Hailesilassie/DW

Ripoti hiyo juu ya "hali ya watoto duniani kwa mwaka 2023" imethibitisha dalili za awali na kuonyesha data zaidi kwamba janga la Covid-19 liliingilia kati "chanjo za utotoni kila mahali". Nusu ya nchi 20 duniani zenye idadi kubwa ya watoto wasiopata chanjo, ikitajwa kama "dozi sifuri" zinapatikana afrika.

Nchini Nigeria, watoto milioni 2.2 hawajawahi kupata chanjo na huko Ethiopia watoto wapatao milioni 1.1 hawana chanjo dhidi ya magonjwa. Ripoti hiyo imetolewa wakati afrika lakini pia maeneo mengine ya ulimwengu yakiripoti milipuko kadha ya magonjwa. Katika nchi ya Kusini mwa Afrika ya Malawi, zaidi ya watu 1000 walifariki kutokana na mlipuko wa kipindupindu mwanzoni kabisa mwa mwaka huu, ukiwa ni mlipuko mbaya katika kipindi cha miaka 20.UNICEF: Watoto milioni 11 wanategemea misaada ya kiutu Yemen

Takribani watoto 700 walifariki kwa mlipuko wa ugonjwa surua huko Zimbabwe mwaka jana. Watoto wengi wa nchi hiyo hawakuwa wamepatiwa chanjo dhidi ya ugonjwa huo kwa mujibu wa taarifa za mamlaka. UNICEF inasema "mahitaji makubwa ya mifumo ya afya, ubadilishaji wa rasilimali za chanjo na kuzielekeza katika chanjo ya COVID-19, uhaba wa wafanyakazi wa afya na hatua za watu kufungiwa nyumbani" vyote vilichangia kukosa chanjo kote ulimwenguni. Inataja pia mizozo, mabadiliko ya tabia nchi na hofu ya kupatiwa chanjo kama sababu nyingine zilizochangia.

Malawi Msumbiji kimbunga Freddy
Maafa ya kimbunga Freddy nchini Malawi na MsumbijiPicha: Thoko Chikondi/AP/dpa/picture alliance

UNICEF inadai kwamba janga hilo lilidhihirisha ukosefu wa uthabiti na udhaifu uliopo katika mifumo ya afya na huduma za msingi za afya barani afrika. Mwaka jana nchi 34 kati ya 54 za afrika zilikabiliwa na milipuko ya magonjwa kama vile surua, kipindupindu na polio. Mkurugenzi wa kanda ya mashariki na kusini mwa afrika wa UNICEF Mohamed M. Fall, alisema kuwa kuibuka tena kwa magonjwa hayo kunapaswa kuwa tahadhari ya wazi kwa afrika.UNICEF: Watoto 1,000 hufa kila siku kwa kunywa maji machafu

Ameongeza kwamba " viongozi wa afrika wanapaswa kuchukua hatua sasa za kisiasa za kupunguza pengo katika utoaji wa chanjo na kuhakikisha kwamba watoto wote wanapatiwa chanjo na kulindwa. UNICEF imetaja kwamba watoto waliozaliwa kabla au wakati wa janga hilo sasa wanapita umri ambao kwa kawaida wangechanjwa na kusisitiza haja ya mamlaka za afya "kushikamana" na wale waliokosa chanjo ili kuzuia milipuko ya magonjwa hatari zaidi.