Unene kupita kiasi waongezeka kwa watoto na vijana duniani
12 Oktoba 2017Ripoti mpya ya Shirika la Afya Duniani, WHO, imebaini kuwa unene kupita kiasi kwa watoto na vijana umeongezeka mara kumi zaidi katika miaka 40 iliyopita hali inayowaweka katika hatari zaidi ya kupata maradhi ya moyo, kisukari na saratani.
Ripoti hiyo imebaini kuwa kuna ongezeko kubwa la unene kupita kiasi kwa vijana na watoto duniani katika kipindi cha miongo minne iliyopita.
Kadhalika ripoti hiyo imesema, asilimia 8 ya watoto wa kiume na 6 wa kike, wana unene kupita kiasi katika nchi zenye uchumi wa chini na wa kati huku tatizo kubwa likionekana katika bara la Asia.
Wakizungumza katika Chuo Kikuu cha Imperial jijini London, wataalamu waliofanya utafiti huo wamesema unene kupita kiasi umeongezeka hata Marekani, Kaskazini mwa bara la Ulaya na katika nchi nyingine tajiri duniani.
Kuna watoto milioni 120 wanene duniani
Kiongozi Mkuu wa Utafiti huo, Majid Ezzati anasema: "Katika kipindi cha miaka 40 kumekuwa na ongezeko la watoto wenye unene kupita kiasi ambapo mpaka sasa wapo 120 milioni duniani. Tunaona kuwa katika nchi maarufu duniani kama China, Mexico, Brazil na Egypt, kuna ongezeko kubwa la hali hii, ongezeko kubwa linalosababisha kuwepo kwa watoto wengi wenye unene kupita kiasi. Sasa ni ipi sababu ya ongezeko hilo, ni kwa sababu ya mabadiliko yasiyo na afya katika lishe."
Ezzati anasema mwaka 1975 watoto wa umri huo hawakuwa na tatizo hilo ukilinganisha asilimia 8 ya watoto wa kiume na asilimia 6 ya wa kike ambao walibainika kuwa na unene usio wa kawaida mwaka 2016.
Utafiti huo ulifanyika kwa watoto na vijana 129 milioni wa umri wa kuanzia mwaka mmoja hadi miaka 19 .
Watafiti hao wameshauri kuwepo kwa mlo bora nyumbani na shuleni na mazoezi ya kutosha ili kuzuia watoto hao kupata maradhi ya kisukari, moyo na saratani kutokana na uzito huo.
WHO imeshauri kuwa watoto waangaliwe katika sukari wanayokula, chumvi na mafuta.
Pia, wameshauri kodi iongezwe na udhibiti wa hali ya juu ufanyike katika vyakula vya mikahawani visivyofuata kanuni za afya bora.
WHO yashauri kuongezwa kodi katika vinywaji
Kadhalika WHO imeshauri kutambulishwa kwa kodi ya asilimia 20 kwa vinywaji vyenye sukari ili kupunguza matumizi yake.
Fiona Bull wa kitengo cha magonjwa yasiyoambukiza cha WHO anashauri mazoezi zaidi kwa watoto wawapo shuleni au nyumbani.
"Watoto hawapewi mazoezi wakiwa shuleni, kuna vyakula vibaya katika shule nyingi, zile tabia za kutembea au kuendesha baiskeli kwenda shule siku hizi hakuna.Hata wazazi hawawapi watoto ushauri mzuri kuhusu lishe," amesema Fiona Bull
Imeelezwa kuwa iwapo hali hiyo itaendelea, ifikapo mwaka 2022 kutakuwepo watoto wengi zaidi wenye unene kupita kiasi na vijana duniani kuliko walio na uzito wa kawaida. Kwa sasa wapo 192, huku nusu yao wakitokea India.
Kwa nchi zenye kipato cha juu, Marekani imeonekana kuwa na idadi kubwa ya watoto wenye uzito mkubwa ikiwa na watoto wa kike asilimia 19.5 wenye tatizo hilo na asilimia 23.3 wa kiume.
WHO imesema sababu kubwa ya ongezeko hilo la watoto wenye unene kupita kiasi ni pamoja na mabadiliko katika aina za vyakula, tabia na kiwango cha chakula.
Mwandishi: Florence Majani/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef