1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNDP: Mbadiliko ya tabianchi yaathiri ukuaji wa uchumi

14 Desemba 2018

Mabadiliko ya tabianchi yanatishia kurejesha nyuma ukuaji wa uchumi na mafanikio ya kijamii yaliyopatikana barani Afrika kwa miongo kadhaa. Taarifa hiyo ni kulingana na ripoti mpya iliyozinduliwa leo na Shirika la UNDP.

https://p.dw.com/p/3A6YD
Weltklimagipfel in Kattowitz
Picha: picture -alliance/NurPhoto/D. Zarzycka

Ripoti hiyo imezinduliwa  kwa ushirikiano na Mpango Unaofaa wa Afrika kwenye mkutano kuhusu hai ya hewa mjini Katowice, Poland, ambao umewaleta pamoja viongozi wa mataifa mbalimbali duniani kujenga kasi ya kuafikia malengo yaliyoratibiwa kwenye Mkataba wa kihistoria wa Paris. Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Naibu Katibu Mkuu wa UNDP eneo la Afrika  Ahunna Eziakonwa amesema mataifa ya Afrika yamekua kiuchumi, kisiasa na katika masuala ya jamii lakini bado kuna tofauti kati ya tajiri na maskini.

Anasema kuwa licha ya umaskini kupungua bado linasalia kuwa suala tete katika mataifa mengi. Na mabadiliko ya tabianchi, ukame, mafuriko na kubadilika kwa mifumo ya mvua na migogoro ina uwezo wa kuharibu jitihada za kupunguza njaa na kuafikia malengo yalitajwa katika mkataba wa Paris. Ripoti hiyo imetathmini juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa zinazofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mipango ya Maendeleo katika muda wa miaka 15 iliyopita pamoja na ufadhili wa taasisi nyingine kama vile Kituo cha Mazingira Duniani.

UN-Klimakonferenz 2018 in Katowice, Polen | Gruppenbild
Picha: picture-alliance/dpa/Keystone/P. Klaunzer

Wakati vigezo vya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi vikionesha uwezo mzuri wa ufanisi wa kiuchumi, kuimarisha maisha na kupunguza hatari barani Afrika, ripoti hiyo imebaini kuwa uendelevu wa muda mrefu utategemea kukithiri wa viwango vya umaskini, mazingira pana ya sera na masharti, upatikanaji wa masoko na huduma za kifedha, pamoja na uwezo wa serikali kutoa msaada wa kiufundi kwa jamii.

Iwapo dunia haitaweza kuafikia malengo yake ya kuhakikisha ongezeko la joto la dunia linabakia chini ya nyuzi joto 2, mataifa ya Afrika huenda yakafikia hatua ya kusonga, kulingana na waandishi wa ripoti hii, wakati changamoto zitaongezeka kwa kiasi kikubwa na vitisho kutokea kutokana na joto jingi. Hatua hiyo ya kusonga ina uwezo wa kusababisha njaa upya na kutatiza juhudi za dunia za kumaliza umaskini na njaa ifikapo mwaka 2030.

Kadhalika kulingana na ripoti hiyo, kwa mara ya kwanza, zaidi ya mwongo mmoja uliopita, njaa duniani imeongezeka, na kuathiri asilimia 11 ya idadi ya watu duniani, kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO.

Mwandishi: Sophia Chinyezi/UNDP

Mhariri: Mohammed Khelef