UN yawahimiza viongozi wa Maziwa Makuu kumaliza mizozo
21 Oktoba 2021Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limewatolea mwito viongozi wa eneo la Maziwa Makuu barani Afrika kutumia fursa ya maendeleo mazuri ya hivi karibuni ya kisiasa ili kumaliza mizozo isiyokwisha pamoja na kuzuia uchimbaji haramu wa dhahabu na mali asili nyengine mashariki mwa Congo.
Taarifa ya pamoja iliyoidhinishwa na chombo chenye nguvu zaidi cha Umoja wa Mataifa imeweka wazi juhudi za kidiplomasia zilizohusisha Marais wa Congo, Rwanda na Burundi ambazo zimefungua njia ya kuboresha ushirikiano wa kikanda kati ya nchi hizo.
Baraza hilo la usalama la Umoja wa Mataifa pia limepongeza juhudi za Umoja wa Afrika na makundi mengine ya kikanda katika kusaidia mchakato wa kisiasa na kutatua migogoro katika eneo la Maziwa Makuu.
Soma pia: NATO yatafakari kusaidia juhudi za amani ukanda wa Sahel-UN
Waziri wa mambo ya nje wa Kenya Raychelle Omamo ambaye aliongoza kikao cha baraza hilo amesema hali inaendelea kuwa shwari katika eneo la Maziwa Makuu kwani kwa sasa kuna ushirikiano mkubwa kati ya mataifa ya ukanda huo na hivyo basi kuepusha uwezekano wa kutokea mivutano. Omamo ameendelea kusema kuwa ushirikiano huo utawezesha mataifa hayo kushughulikia changamoto ya migogoro, umaskini na maendeleo duni.
Waziri huyo wa mambo ya nje wa Kenya amesema, "Uhusiano kati ya maliasili na migogoro bado unasalia changamoto kuu kwa nchi nyingi za Maziwa Makuu."
UN yaipongeza Umoja wa Afrika katika kusaidia mchakato wa kisiasa eneo la Maziwa Makuu
Naye mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa kanda ya Maziwa Mkuu Huang Xia ameliambia baraza hilo kuwa mashauriano ya mawaziri pamoja na ziara za mara kwa mara za kiserikali katika muda wa miezi sita iliyopota, zimefungua njia ya mahusiano mema kati ya nchi za ukanda huo.
Xia ameongeza kusema kuwa mashauriano hayo pia yamefufua ushirikiano katika masuala ya usalama, biashara, miundo mbinu, kawi na mali asili.
Soma pia: Umoja wa Mataifa hatiani kuhusu unyanyasaji wa kingono DRC
Mjumbe huyo maalum wa Umoja wa Mataifa kwa kanda ya Maziwa Makuu hata hivyo ametahadharisha kuwa, licha ya mafanikio hayo harakati za makundi ya wenye silaha bado zinatishia amani na usalama katika eneo hilo.
Kadhalika, naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Afrika, Martha Pobee ameliambia baraza hilo kuwa Umoja wa Mataifa umetiwa moyo na hali ya ushirikiano kati ya nchi za Maziwa Makuu. Bi. Pobee hata hivyo ameunga mkono kauli ya Huang Xia kuwa makundi yenye silaha yanayoendesha oparesheni zake mashariki mwa Congo yanatishia kuvuruga mafanikio yaliyopatikana hadi sasa.