1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yatoa wito wa majadiliano Zimbabwe

Mtullya, Abdu Said1 Julai 2008

Viongozi wa Umoja wa Afrika watakiwa kutatua mgogoro wa Zimbabwe.

https://p.dw.com/p/ETvl
Rais Hosni Mubarak wa MisriPicha: AP

Umoja wa Mataifa umewataka viongozi wa Afrika wanaokutana kwenye kitongoji cha mapumziko cha Sharm- el- Sheikh nchini Misri watatue mgogoro wa Zimbabwe.Akizungumza kwenye mkutano wa viongozi hao,naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Asha-Rose -Migiro amesema mkutano huo ni wasaa wa ukweli. Ameeleza kuwa viongozi wengi wamepaaza sauti zao juu ya suala la Zimbabwe.Bibi Asha-Rose -Migiro pia ametoa mwito juu ya kufanyika mdahalo baina ya pande zote nchini Zimbabwe,kwa kuungwa mkono na Umoja wa Afrika na wahusika wengine barani Afrika, ili kurejesha amani na utengemavu nchini humo.


Viongozi wa Umoja wa Afrika leo pia wanatarajiwa kusisitiza umuhimu wa kufanyika mazungumzo baina ya rais Robert Mugabe na wawakilishi wa upinzani.

Lakini hakuna matarajio makubwa juu ya viongozi wa Umoja wa Afrika kuchukua hatua za kuuadhibu utawala wa Mugabe kwa sababu ya kufanya uchaguzi ambao hakuwa halali wala huru.

Wakati huo huo Marekani inatayarisha mswada wa azimio juu ya kuiwekea Zimbabwe vikwazo vya Umoja wa Mataifa.Vikwazo hivyo vinalenga kupiga marufuku kuiuzia silaha Zimbabwe na kuzuia mali za watu na kampuni fulani.