UN yataja kampuni zenye mafungamano na walowezi wa Kiyahudi
13 Februari 2020Msemaji wa Ofisi ya Kamishna mkuu wa Haki za Binadamau wa Umoja wa Mataifa, Rupert Colville amesema ripoti hiyo imeziainisha shughuli makhsusi za kibiashara zinazogusa haki za wapalestina, lakini akatahdharisha kwamba haikuzitaja kampuni hizo 112 kama haramu.
Kwa zaidi ya nusu karne sasa, Israel imekuwa ikitekeleza sera ya ujenzi ya makaazi ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi, ujenzi ambao jumuiya ya kimataifa inauchukulia kuwa kinyume cha sheria.
"Ni muhimu kuweka wazi kwamba hii siyo orodha nyeusi kama baadhi wanavyodai, na wala haifanyi shughuli za kampuni yoyote kuwa haramu," alisema Rupert Colville.
Netanyahu aapa kutwa maeneo zaidi
Akiimarishwa na mpango mpya wa rais wa Marekani kuhusu amani ya Mashariki ya Kati, waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameapa kutwaa makaazi mengine zaidi ya 100, wakati ambapo mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC, akiashiria kuwa atafungua hivi karibuni, uchunguzi wa uhalifu wa kivita kuhusiana na sera za ulowezi za Israel.
Orodha hiyo inajumlisha makampuni makubwa ya kimataifa, miongoni mwake yakiwemo Airbnd, Motorola na General Mills. Ingawa sehemu kubwa ya dunia inayazingatia makaazi ya walowezi kuwa haraam, ripoti hiyo ya jana haikuyatuhumu makampuni hayo kwa kuvunja sheria ya kimataifa.
Badala yake, ilionekana kulenga kuyatia kishindo kwa kuvutia nadhari hasi juu ya uhusiano wake na sera ya Israel inayochukiwa.
Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet, alisema anafahami fika kwamba suala hilo ni tete na litaendelea kuwa tete, lakini akaongeze akuwa wameridhika kwamba ripoti yao inaakisi uzingativu mkubwa uliopewa kwa uchunguzi huo.
Baraza la Haki za Binadamu liliiagiza ofisi ya haki za binadamu mwaka 2016, kuunda hifadhi ya data ya makampuni yanayohusiana au yanayounga mkono ujenzi wa makaaazi ya walowezi.
Vigezo vya kuorodheshwa
Orodha hiyo iliyoanza na makampuni zaidi ya 300, ilipunguzwa hadi kufikia 112, ambayo yanajihusisha na vitendo vinavyosababisha wasiwasi wa haki za binadamu, kama vile ujenzi wa makaazi ya walowezi, huduma za ulinzi, benki na vifaa vilivyotumiwa kuvunja majumba ya Wapalestina.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amelaani ripoti hiyo na kulituhumu baraza la haki za binadamu kwa upendeleo, akidai kuwa badala ya kushughulikia haki za binadamu, baraza hilo linajaribu kuchafua jina la Israel.
Waziri wa mambo ya nje wa Palestina Riad Malki kwa upande wake aliisifu ripoti hiyo kama ushindi wa sheria ya kimataifa na wa juhudi za kidiplomasia kukausha vyanzo vya mfumo wa kikoloni unaowakilishwa na makaazi haraamu ya walowezi katika ardhi ya Wapalestina.
Chanzo: Mashirika