UN yaonya kuhusu matumizi mabaya ya maji
23 Machi 2023Akizungumza katika mkutano wa kwanza wa Umoja wa Mataifa kuhusu maji ambao umeandaliwa baada ya karibu nusu karne, Katibu Mkuu Antonio Guterres amesema ulimwengu unauangamiza ubinaadamu kupitia matumizi kupita kiasi ya maji na yasiyo endelevu. "Tumevunja mzunguko wa maji, tumeharibu mifumo ikolojia na kuchafua maji ya chini ya ardhi. Takriban majanga matatu kati ya manne ya asili yanahusishwa na maji. Mtu mmoja kati ya wanne anaishi bila huduma za maji zinazosimamiwa kwa usalama au maji safi ya kunywa. Na zaidi ya watu bilioni 1.7 hawana huduma za msingi za usafi.”
Soma pia: UN: 26% ya watu duniani hawana maji safi
Kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na mazingira safi ni sehemu ya orodha ya mambo 17 ya kufanywa ambayo Umoja wa Mataifa umeweka kwa ajili maendeleo endelevu, pamoja na kumaliza njaa na umaskini, kufikia usawa wa jinsia, na kuchukua hatua kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
Soma pia: UNICEF: Watoto 1,000 hufa kila siku kwa kunywa maji machafu
Mkutano huo wa siku tatu ulioanza jana mjini New York haunuii kutoa aina ya muafaka wa kisheria ambao ulifikiwa katika mikitano ya tabia nchi ya Paris mwaka wa 2015, au mkakati kama uliowekwa kwa ajili ya ulinzi wa mazingira asili mjini Montreal mwaka wa 2022.
Badala yake, lengo ni kutengeneza kile kinachofahamika kama Ajenda ya Kuchukua Hatua kujusu Maji, ambayo itakuwa na ahadi za hiari na kutengeneza msukumo wa kiasiasa.
Soma pia: UN: Uhaba wa maji watishia mzozo wa kimataifa
Guterres ametoa wito wa kuwepo uwekezaji mkubwa katika maji na mifumo ya usafi na juhudi za kushughulikia mabadiliko ya tabia nchi, akisisitiza kuwa mambo hayo mawili yanaenda sambamba. "mkutano huu lazima uonyeshe hatua kubwa katika uwezo wa Mataifa wanachama na jamii ya kimataifa kutambua na kuchukua hatua kuhusu umuhimu wa maji kwa ulimwengu wetu nak ama chombo cha kukuza amani na ushirikiano wa kimataifa"
Tayari Zaidi ya ahadi 500 zimewasilishwa kutoka kwa serikali mbalimbali, mashirika ya Umoja wa Mataifa, viongozi wa kibiashara na mashirika ya kijamii.
Marekani imesema itawekeza dola bilioni 49 katika miradi ya maji na usafi ndani na kote ulimwenguni.
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Linda Thomas-Greenfield amesema fedha hizo zitasaidia kutenegeneza ajira, kuzuia migogoro, kulinda afya ya umma, kupunguza kitisho cha uhaba mkubwa cha chakula na njaa, na kuwezesha kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na maafa ya kiasili.
Hakutoa ratiba ya uwekezaji huo wala maelezo kuhusu ni kiasi gani cha fedha kitakachotimika wapi.
Shirika la misaada la Oxfam linasema zaidi ya watu milioni 33 hawana maji ya kutosha ya kunywa katika eneo la Afrika Mashariki. Katika maeneo ya Somalia, kaskazini mwa Kenya na kusini mwa Ethiopia, hadi asilimia 90 ya visima katika maeneo ya mashinani, ambavyo ni muhimu katika maisha ya watu, vimekakuka kabisa.
Mkutano huo wa Umoja wa Mataifa kuhusu Maji unaandaliwa kwa Pamoja na Mfalme Willhem-Alexander wa Uholanzi na Rais wa Tajikstan Emomali Rahmon. Kuna nchi 171, wakiwemo zaidi ya mawaziri 100, kwenye orodha ya wazungumzaji.
afp, ap, reuters, dpa