1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yalaani Korea Kaskazini kurusha kombora anga ya Japan

30 Agosti 2017

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani kitendo cha Korea Kaskazini kurusha kombora lililopita katika anga ya Japan kuitaka isitishe majaribio ya makombora na mipango yake ya nyuklia.

https://p.dw.com/p/2j40F
USA UN-Sicherheitsrat in New York - Sondersitzung zu den Rakektentests in Nordkorea
Picha: Reuters/A. Kelly

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikutana jana, baada ya Japan kuomba kikao cha dharura kifanyike ili kuiwekea shinikizo zaidi serikali ya Korea Kaskazini. Marekani iliandaa taarifa ambayo ilikubaliwa pia na China na Urusi, ikisema kuwa kitendo cha Korea Kaskazini kinadhoofisha kwa makusudi amani na utulivu katika ukanda huo na kimesababisha kuwepo kwa wasiwasi mkubwa kuhusu usalama ulimwenguni kote.

Baraza hilo kwa kauli moja ambalo limekiita kitendo cha Korea Kaskazini cha ''kuchukiza'', limeitaka nchi hiyo kuchukua hatua madhubuti na za haraka kupunguza wasiwasi katika Rasi ya Korea na nje ya ukanda huo. Hata hivyo, taarifa hiyo ya Marekani haikutaja haja ya kuiwekea nchi hiyo vikwazo vyovyote vipya.

Akizungumza baada ya mkutano huo, Balozi wa Japan katika Umoja wa Mataifa, Koro Bessho amesema kuanzia sasa watajadiliana hatua zinazofuata. Amesema kwa sasa taarifa hiyo inapeleka ujumbe mzito kwa Korea Kaskazini kwamba jumuiya ya kimataifa haitokubali tabia yake ya uchokozi.

Korea Kaskazini sio mwanachama

Korea Kaskazini sio mwanachama wa baraza hilo lenye wanachama 15. Wakati mkutano huo ukiendelea mjini New York, shirika la habari la Korea Kaskazini lilitangaza kuwa kiongozi wa nchi hiyo, Kim Jong Un ameridhishwa sana na jaribio la kombora lililorushwa jana na kupita katika anga ya Japan na ameamuru kufanyika majaribio zaidi ya makombora kuelekea katika kisiwa cha Guam kinachomilikiwa na Marekani kwenye Bahari ya Pasifiki.

Infografik Timeline Nordkoreas Raketentests 05.07.2017 ENG
Picha inayoonyesha muda ambao Korea Kaskazini imerusha makombora yake

Kwa mujibu wa shirika hilo, Kim alikuwepo kushuhudia wakati kombora hilo la masafa ya wastani chapa Hwasong-12 liliporushwa jana asubuhi na kupita katika anga ya Japan, kabla ya kutua baharini.

Viongozi wa Japan na Korea Kusini wazungumza

Wakati hayo yakijiri, Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe na Rais wa Korea Kusini, Moon Jae In, leo wamekubaliana kuongeza shinikizo kwa Korea Kaskazini. Msemaji wa rais wa Korea Kusini, Park Soo-hyun, amesema viongozi hao wawili waliozungumza kwa njia ya simu pia wameapa kulishinikiza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuweka vikwazo vikali zaidi dhidi ya Korea Kaskazini.

''Rais Moon amemwambia Abe kwamba kombora la masafa ya wastani lililorushwa na Korea Kaskazini na kupita katika anga ya Japan ni zaidi ya uchokozi na ghasia dhidi ya nchi jirani na kwamba serikali ya Korea Kusini imeitisha haraka mkutano wa baraza la usalama wa taifa, kulaani vikali kitendo hicho,'' alisema Park

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Sigmar Gabriel amelaani kitendo cha Korea Kaskazini na ameahidi kuunga mkono juhudi za kidiplomasia za Marekani kuishinikiza Korea Kaskazini kurejea katika meza ya mazungumzo.

Naye Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May ameitaka China kuongeza shinikizo zaidi kwa Korea Kaskazini ili iache kufanya majaribio ya makombora na kwamba China ina jukumu muhimu la kuchukua katika juhudi za kimataifa kuzuia kile alichokielezea kama uchokozi mkubwa unaofanywa na Korea Kaskazini. May ameitoa kauli hiyo akiwa njiani kuelekea Japan kukutana na Abe.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AP, DPA, AFP
Mhariri: Caro Robi