1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yaanzisha uchunguzi wa uvunjaji wa haki za binadamu Libya

30 Oktoba 2020

Shirika la UN limeanzisha kamisheni maalum ya kuchunguza uvunjwaji wa haki za binadamu unaoendelea nchini Libya. Suala hilo limetokea baada ya makaburi ya halaiki kupatikana nchini humo.

https://p.dw.com/p/3kf7Q
Chile, Santiago I Michelle Bachelet und Angela Jeria
Picha: picture-alliance/AP/L. Hidalgo

Makaburi hayo ya halaiki, yaliyozikwa miili ya watu zaidi ya 200, yaligunduliwa miezi sita iliyopita. Ugunduzi wa makabuli hayo umepelekea Shirika la Umoja wa Mataifa linalojishughulisha na haki za binadamu la OHCHR, kuanzisha  timu itakayochunguza uvunjwaji wa haki za binadamu nchini Libya, pamoja na watu wanaosadikiwa kufanya mauji hayo ya watu waliozikwa katika makaburi ya halaiki.

Moja ya kazi inayotakiwa kufanywa na kamisheni hiyo ni kutafuta watu waliofanya madhila hayo tokea mzozo wa Libya ulipoanza mwaka 2014. Kiongozi wa kamisheni hiyo ya Umoja wa Mataifa unaojishughulisha na haki a binadamu, Michelle Bachelet, alisema kwamba kamisheni hiyo itafanya juu chini kuzuia migogoro na kuleta amani na utulivu katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Ingawa kuna harakati hizo za Shirika la Umoja wa Mataifa za kuhakikisha wahalifu wanapatikana na kuwekwa hatiani, ni walibya wachache wanaoona kwamba jitihada hizo zitazaa matunda.

Libyen Unruhen Proteste
Raia wa Libya wazua ghasia mjini BenghaziPicha: Hakeam el-Yamany/AP Photo/Picture-alliance

Anas, ambye ni raia wa Libya kutoka Benghazi ana wasiwasi kama uchunguzi huo wa Shirika la Umoja wa Mataifa utasaidia kuleta amani, kwani serikali zote mbili zinazogombania madaraka sasa zinasadikiwa kuhusika katika uvunjwaji huo wa haki za binadamu. Tokea machafuko yalipotokea miaka sita iliyopita, Libya imegawanyika katika makundi mawili, lile la nyumba ya wawakilishi ya Tobruk, iliyochaguliwa mwaka 2014, na kwa upande mwingine, ni ile serikali ya umoja wa kitaifa inayoungwa mkono na shirika la Umoja wa Mataifa, iliyoundwa mwaka 2016.

Wapiganaji na wafuasi wanaounga mkono pande hizo mbili za serikali, wote wanatuhumiwa kufanya madhila hayo katika kuvunja haki za binadamu, hivyo ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa itabidi ihusishe pande hizo mbili katika uchunguzi wao. Jelel Harchaoui mtafiti kutoka Libya wa Taasis ya Clingendael iliyopo Uholanzi alisema kwamba shirika la Umoja wa Mataifa inabidi lijiangalia na kujiuliza kama kweli linaweza kusaidia kuleta amani katika nchi hiyo na kuwaunganisha watu wote. 

Walioteuliwa kufanya uchunguzi huo wapo kwenye presha kubwa, kwani wanatakiwa kuhakikisha ripoti watakayoitoa haita vuruga majadiliano ya amani yanayoendelea hivyi sasa nchini Libya. Mpaka kufikia mwezi wa Novemba mwaka 2021, matokeo ya awali ya uchunguzi wao yanatakiwa kufikishwa kwa shirika la kutetea haki za binadamu la Umoja wa Mataifa.