1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Watu 190,000 wanahitaji msaada wa haraka Indonesia

1 Oktoba 2018

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na uratibu wa masuala ya kibinaadamu, OCHA limeonya kuwa kiasi ya watu 190,000 wa Indonesia wanahitaji msaada wa dharura wa kibinaadamu kutokana na matetemeko ya ardhi na tsunami.

https://p.dw.com/p/35p3v
Indonesien nach dem Tsunami in Palu
Picha: Reuters

Taarifa ya shirika hilo iliyotolewa leo, imeeleza kuwa idadi hiyo inawajumuisha watoto wapatao 46,000 na watu wazima 14,000, wengi wakiwa nje ya mji ambako serikali haijaelekeza sana juhudi zake za uokozi. Tangazo hilo la Umoja wa Mataifa limetolewa wakati ambapo Indonesia inapambana na shughuli za uokozi, baada ya kisiwa cha Sulawesi kukumbwa na matetemeko ya ardhi pamoja na kimbunga cha tsunami. 

Msemaji wa idara ya majanga ya kitaifa na uokozi nchini Indonesia, Sutopo Nugroho anasema miundombinu mibovu inakwamisha shughuli za uokozi na kwamba mashirika ya kibinaadamu yanajaribu kuwaondoa watu katika maeneo yaliyoathirika.

Indonesien Das Roa-Roa Hotel auf Sulawesi nach dem Erdbeben
Waokoaji wakiendelea na shughuli za uokoziPicha: REUTERS

''Tunakabiliwa na vizingiti vingi katika mchakato mzima wa kuwaondoa watu, ikiwemo ukosefu wa umeme, mawasiliano hafifu, uhaba wa vifaa vinavyofaa vya uokozi na idadi ndogo ya wafanyakazi. Na bado mamia ya watu wamekwama katika kifusi cha majengo yaliyoporomoka na wengine kadhaa wamezikwa kwenye matope,'' alisema Nugroho.

Inaaminika kuwa watu wengi wamekwama katika hoteli kadhaa na eneo la maduka makubwa kwenye mji wa Palu, uliopo umbali wa kilomita 1,500 kaskazini mashariki mwa Jakarta.

Awali Rais wa Indonesia, Joko Widodo aliomba msaada wa dharura wa kimataifa ili kusaidia kuyaokoa maisha ya watu, lakini serikali yake imesema walikuwa katika hali ya kuchanganyikiwa na masikitiko na kwamba hali imedhibitiwa.

Kiasi ya nchi 18 na mashirika kadhaa ya misaada yalijitolea kusaidia tangu majanga hayo yaliyopotokea siku nne zilizopita, lakini hadi sasa hayajafanikiwa kufanya hivyo. Idadi ya watu waliokufa hadi sasa ni 884 na inatarajiwa kuongezeka zaidi.

Erdbeben und Tsunami in Indonesien
Watu wakisubiri kuondolewa kwenye maeneo yaliyoathirikaPicha: Reuters/Antara Foto

Wakati hayo yakijiri, kituo cha utafiti wa kijiolojia cha Ujerumani kimesema mashirika yanayohusika na uratibu wa majanga nchini Indonesia yalishindwa kutoa tahadhari kuhusu tsunami. Joern Lauterjung, Mkurugenzi wa shughuli za kijiolojia, amesema kuwa tatizo kubwa lilikuwa ni mawasiliano kati ya mamlaka za ndani pamoja na watu.

Wakati huo huo, Waziri Wiranto anayehusika na Usalama wa ndani wa Indonesia, amewataka kiasi ya wafungwa 1,200 waliotoroka kwenye magereza matatu ya Palu na Donggala yaliyoharibiwa na matetemeko hayo pamoja na tsunami kujisalimisha ndani ya wiki moja.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, DPA, AP, Reuters
Mhariri: Mohammed Abudl-Rahman