UN: Wasyria wanaorejea nyumbani wanakabiliwa na unyanyasaji
13 Februari 2024Ripoti hiyo iliyoandaliwa na Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imekusanya ushuhuda wa Wasyria waliorejea nyumbani ambao wametoa taswira ya hali ya kutisha wanayokabiliana nayo kwenye nchi hiyo.
Imekusanya simulizi za unyanyasaji na mateso ikiwemo watu kukamatwa bila makosa na kudhulumiwa kingono, vitendo ambavyo vinatuhumiwa kufanywa na maafisa wa serikali ya Syria.
Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk, amesema taswira halisi ya hali nchini Syria imetolewa kupitia ripoti hiyo katika wakati idadi ya Wasyria wanaolazimishwa kurejea nchini mwao kutoka mataifa mengine inaongezeka.
Syria ilitumbukia vitani tangu mwaka 2011 kufuatia maandamano ya umma ya kutaka kuung'oa utawala wa rais Bashar al-Assad bila mafanikio.