1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Wasyria milioni 13 wanahitaji msaada wa haraka

31 Oktoba 2017

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana limearifiwa masuala mbalimbali na kupokea taarifa kadhaa kuhusu mzozo wa Syria, vita dhidi ya ugaidi katika ukanda wa Sahel pamoja na mzozo wa Rohingya.

https://p.dw.com/p/2mn4y
Schweiz Mark Lowcock in Genf
Mark Lowcock (Katikati) akiwa na wakuu wa mashirika mengine ya UNPicha: picture-allianvce/AP Photo/S. Di Nolfi

Mkuu wa masuala ya kibinaadamu wa Umoja wa Mataifa, Mark Lowcock ameliambia Baraza la Usalama la umoja huo kwamba zaidi ya Wasyria milioni 13 wanahitaji msaada wa haraka ili kuyaokoa maisha yao. Amesema vita vimesababisha watu kukosa makaazi na upatikanaji mdogo wa chakula, huduma za afya na mahitaji muhimu, ingawa Umoja wa Mataifa unashirikiana na washirika wao kuendelea na juhudi hizo nchini Syria.

''Tunawafikia mamilioni ya watu kwa mwezi mmoja. Kwa mfano mwezi Septemba, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP lilitoa msaada wa chakula kwa zaidi ya watu milioni 3.3, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto, UNICEF liliwafikia zaidi ya watu milioni 1.5 na Shirika la Afya Duniani, WHO liliwafikia zaidi ya watu 800,000,'' alisema Lowcock.

Türkei Syrien Grenze bei Akcakale
Wakimbizi wa SyriaPicha: Getty Images/G. Sahin

Lowcock amesema idadi ya watu wasio na makaazi nchini Syria imepungua kwa muda mrefu kutoka milioni 6.3 hadi milioni 6.1, lakini viwango vipya vya watu wasio na makaazi bado viko juu, huku watu milioni 1.8 wakiripotiwa kulazimika kuyakimbia makaazi yao kati ya mwezi Januari na Septemba.

Tangu kuanza kwa operesheni za kijeshi Novemba, 2016 ambazo zimewaondoa wapiganaji wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS kutoka kwenye mji wa Raqqa, mashambulizi ya anga na mapigano yamesababisha zaidi ya watu 436,000 kuyakimbia makaazi yao na kwenda katika maeneo 60 tofauti.

Watu milioni 3 wako kwenye maeneo yaliyozingirwa

Lowcock amesema karibu watu milioni tatu wanaendelea kuishi katika maeneo yaliyozingirwa na maeneo ambayo ni magumu kufikiwa, ambako Umoja wa Mataifa unakabiliana na changamoto kubwa kufanya shughuli zake za kutoa msaada wa kibinaadamu.

Wakati huo huo, Marekani imeahidi kutoa Dola milioni 60 ili kuunga mkono kikosi kinachopambana na ugaidi katika ukanda wa Sahel Afrika Magharibi, ambako ghasia zinazoungwa mkono na wanamgambo wa IS zimesababisha zaidi ya watu milioni 5 kukosa makaazi. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Rex Tillerson ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba fedha hizo zitakuwa maalum kwa ajili ya kufikia amani katika ukanda huo ulioharibiwa.

Gipfeltreffen in Bamako Mali
Viongozi wa nchi za Ukanda wa Sahel katika mkutanoPicha: Reuters/L. Gnago

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Nikki Haley amesema nchi za Burkina Faso, Chad, Mali, Mauritania na Niger zinazounda kikosi hicho cha kupambana na ugaidi, zinapaswa kuchukua udhibiti kamili wa kikosi hicho. Haley anaonekana kulipuuza pendekezeo lililotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres la kuanzisha ofisi ya umoja huo kwenye ukanda wa Sahel, ambayo itasaidia kufatilia shughuli zinavyoendeshwa na hasa kulinda haki za binaadamu.

Ama kwa upande mwingine Umoja wa Mataifa umemteua Knut Ostby kutoka Norway kuwa mratibu mpya wa mpito kwa ajili ya Myanmar ambapo atakuwa na jukumu la kushughulikia misaada ya kibinaadamu katika wakati ambapo matatizo yanaongezeka kati ya serikali ya Myanmar kutokana na jinsi inavyoushughulikia mzozo wa Rohingya.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AP, Reuters
Mhariri: Caro Robi