UN: Vita vya Syria vinazidi kuongezeka
4 Mei 2018Mshauri wa masuala ya kibinaadamu wa Umoja wa Mataifa, Jan Egeland amesema kuwa mamilioni ya raia bado wamekwama katika mzozo wa Syria uliodumu kwa miaka saba na wengi wao ambao wamekimbia kwenye maeneo ya mapambano wanatafuta makaazi kwenye kambi ambazo zimefurika kwenye jimbo la Idlib lililoko kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.
''Ningependa kusema hofu yetu namba moja ni kwamba kuna raia wengi wanaoishi kwenye mazingira ya hatari. Kuna mara sita zaidi ya raia Idlib na wanaishi kwa taabu sana. Wanaishi kwenye maeneo ya wazi, wanaishi kwenye kambi za watu wasio na makaazi ambazo zimefurika. Hivyo hatuwezi kuwa na vita Idlib,'' alisema Egeland.
Egeland amesema kiasi ya Wasyria 11,000 bado wamezingirwa na watu milioni mbili wanapata shida kuifikia misaada ya kibinaadamu, ikilinganishwa na watu 625,000 waliozingirwa na watu milioni 4.6 ambao walipata shida kuifikia misaada ya kibinaadamu kwa mwaka mmoja uliopita.
Egeland amesema ameziambia Urusi, Iran, Uturuki na Marekani kwamba kuzuka kwa mapigano mapya Idlib litakuwa janga baya zaidi kwa raia na ametoa wito wa kufanyika mazungumzo ya kuwalinda raia na ameonya kuhusu mashambulizi ya anga ya hivi karibuni Idlib.
Katika mkutano wa wafadhili uliofanyika wiki iliyopita mjini Brussels wafadhili wa kimataifa walichanga Dola bilioni 4.4 za msaada wa dharura kwa ajili ya Syria na majirani zake, lakini kiasi hicho hakikufikia lengo la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya mwaka 2018, baada ya Marekani kushindwa kuwasilisha mchango wake iliyoahidi.
Hofu ya waasi
Wapiganaji wanasema wanahofia mashambulizi mapya katika jimbo la Idlib yatakayofanywa na jeshi la serikali ya Syria pamoja na washirika wao Urusi na Iran. Waasi hao wanasema mashirika ya misaada yamebainisha kuwa mashambulizi hayo yanaweza kusababisha hatari kubwa zaidi kwa raia kadhaa ikilinganishwa na watu waliozingirwa mwaka uliopita mjini Aleppo.
Hayo yanajiri wakati ambapo leo waasi wa Syria wameendelea kusalimisha silaha zao za kivita baada ya kufikia makubaliano mapya na serikali. Shirika linalofuatilia haki za binaadamu nchini Syria lenye makao yake mjini London, Uingereza, limesema kuwa wapiganaji hao wanakabidhi silaha hizo kwa vikosi vya Urusi na vya serikali ya Syria kwa siku ya pili mfululizo.
Mapema wiki hii, waasi wa Syria walikubaliana na vikosi vya serikali pamoja na washirika wao kusitisha mapigano kwenye maeneo ya majimbo ya kati ya Syria ya Hama na Homs, ikiwemo miji ya waasi ya Talbisseh, Rastan na Al-Houla.
Wakati huo huo, kiasi ya watu wawili akiwemo mfanyakazi wa Kamati ya Msalaba Mwekundu duniani, wameuawa katika shambulizi la bomu lililotokea kwenye eneo la Dana, Idlib jana.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef