1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Vikwazo vya silaha nchini Libya havikuleta tija

17 Machi 2021

Wataalamu sita wa UN waliopewa jukumu la kufuatilia vikwazo vya silaha nchini Libya wameyalaumu mataifa ya nje yanayounga mkono pande mbili zinazozozana nchini humo pamoja na mamluki na makundi yasiokuwa ya serikali .

https://p.dw.com/p/3qjSB
Mitglieder des Sicherheitsrates der Vereinten Nationen halten zu Beginn einer Sitzung über Afghanistan im Hauptquartier der Vereinten Nationen im Stadtbezirk Manhattan in New York City eine Schweigeminute ein
Picha: Reuters

Katika ripoti hiyo ya kurasa 550, inayoelezea matukio nchini Libya kutoka mwezi Oktoba mwaka 2019 hadi Januari 2021, wataalamu hao wametumia picha, michoro na ramani kutilia mkazo mashtaka yao.

Ripoti hiyo imeendelea kusema kuwa udhibiti wa pande hizo mbili zinazozozana nchini libya katika usambazaji wa bidhaa, unafanya kuwa vigumu kutambua, kuingilia ama kuweka vizuizi na ikaelezea kuwa pande zote mbili zinafanya utekelezaji wa vikwazo hivyo  kuwa vigumu zaidi. Wataalamu hao wanakadiria kuwa kiasi cha mamluki elfu mbili wa kundi la Wagner wamepelekwa nchini Libya nakwamba Pamoja na makubaliano ya Oktoba 25 mwaka 2020 yakusitisha mapigano, hakujakuwa na dalili za kundi hilo kutoka Libya.

Kampuni nyingine ya kibinafsi ya Urusi, Rossiskie System Bezopasnosti pia imetajwa kwa jukumu lake la kuzifanyia ukarabati ndege za vita huku shirika la Uturuki la kutoa kandarasi za kijeshi la SADAT ambalo limekanusha kuhusika katika shughuli zozote haramu nchini Libya pia likiwa katika orodha ya walioshtakiwa.

Libyen I Abdul Hamid Dbeibah
Waziri mkuu wa Libya- Abdul Hamid DbeibahPicha: Mucahit Aydemir/AA/picture alliance

Wataalamu hao waliafiki maamuzi sawa kuhusu suala la vikwazo vya kiuchumi vilivyoelekezwa kwa watu binafsi au mashirika wakitaja muendelezo wa ukosefu wa uwazi. Wataalamu hao wamependekeza kuwa baraza la usalama la Umoja huo lifute usajili wa bendera, kuweka marufu ya kupaa na kutua dhidi ya ndege zilizotambuliwa kukiuka vikwazo hivyo.

Pia wamelitaka baraza hilo kutoa idhini kwa mataifa wanachama wake kukagua meli katika bahari kuu ya Pwani ya Libya ambazo wanasababu za kuamini zinasafirisha ama kujaribu kusafirisha nje mafuta ambayo hayajasafishwa ama bidhaa nyingine za mafuta yaliosafishwa. Ripoti hiyo pia imesema kuwa kiasi cha washirika watatu wa mazungumzo ya amani yalioandaliwa nchini Tunisia mnamo mwezi Novemba na kudhaminiwa na Umoja huo walipewa hongo kumpigia kura mwaniaji wa kiti cha waziri mkuu.

Wiki iliyopita, bunge nchini Libya liliidhinisha serikali ya Umoja itakayoongozwa na waziri mkuu Abdul Hamid Dbeibeh aliyeapishwa siku ya Jumatatu.