1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

UN: Sudan yakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula

28 Juni 2024

Ripoti ya Umoja wa Mataifa imesema takriban watu milioni 26 katika nchi iliyokumbwa na vita ya Sudan wanakabiliwa na viwango vya juu vya "uhaba mkubwa wa chakula."

https://p.dw.com/p/4heGN
Sudan-Agari
Watu wamepanga foleni kujiandikisha kwa ajili ya kupokea msaada wa chakula katika kambi ya wakimbizi wa ndani huko Agari Sudan.Picha: Guy Peterson/AFP

Ripoti iliyoandaliwa kwa kutumia kipimo cha kuboresha tathmini ya usalama wa upatikanaji wa chakula na mchakato wa kupitisha maamuzi, Integrated Food Security Phase Classification, IPC imerekodi kwamba katika miezi kumi na nne ya mzozo, Sudan inakabiliwa na viwango vibaya zaidi vya uhaba wa chakula.

Aidha ripoti hiyo imedokeza kwamba mgogoro huo unatarajiwa kuathiri takriban watu milioni 25.6, pamoja na wengine 755,000 wakiwa katika hali ya njaa na milioni 8.5 zaidi wanaokabiliwa na hali ya "dharura".

Imeashiria kuzorota kwa kasi kwa hali ya usalama wa chakula ikilinganishwa na takwimu za awali zilizochapishwa mwezi Disemba, na ongezeko la asilimia 45 la watu wanaokabiliwa na viwango vya juu vya uhaba wa chakula.

Sudan
Mtoto akichota maji katika mto Gash.Picha: AFP/Getty Images

Soma pia: Pande hasimu Sudan zatumia njaa kama silaha - Wataalamu UN

Ripoti hiyo ya IPC imesema mgogoro huo sio tu umesababisha kuhama kwa watu wengi na kuvuruga njia za usambazaji lakini pia umepunguza kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa misaada muhimu ya kibinadamu, na hivyo kuzidisha hali kuwa mbaya zaidi.

Eddie Rowe, Mkurugenzi wa Shirika la WFP nchini Sudan amesema:

"Tuko katika mbio dhidi ya wakati, sio tu kuwa na rasilimali za kutosha, lakini pia kuweza kufikisha rasilimali hizi kwa watu ambao wako kwenye athari ya kufa njaa. Na unapozungumzia janga kubwa zaidi la njaa duniani tunaangalia nusu ya nchi, zaidi ya Wasudan milioni 25 wameainishwa kuwa na uhaba mkubwa wa chakula. Ikiwa tunaweza kufika na kufadhili, tutaweza kuepusha njaa moja kwa moja.”

Maeneo mengi yako hatarini

Vurugu zauwa watu 38 El-Fashir Sudan

Ripoti ya IPC imeeleza kuwa maeneo 14 ya nchi, ambayo ni makazi ya mamilioni ya watu, yalikuwa "katika hatari ya njaa" ambayo inaweza kushika kasi kati ya Juni na Septemba 2024 sanjari na msimu wa mvua ambao unatenga zaidi maeneo ya mbali.

Mikoa hiyo ni pamoja na El-Fasher iliyozingirwa huko Darfur Kaskazini, sehemu za mji mkuu Khartoum na vituo muhimu vya wakimbizi vya Darfur na Kordofan Kusini ambavyo viliathiriwa zaidi na mapigano ya moja kwa moja.

Soma pia: Msaada wa chakula waongezeka Darfur lakini hautoshi - WFP

Ripoti ya IPC inajiri siku moja baada ya wataalam wa Umoja wa Mataifa kushutumu Vikosi vya Wanajeshi vya Sudan vya Burhan na wanamgambo wa RSF kwa "kutumia chakula kama silaha na kuwanyima chakula raia ".