1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita dhidi ya IS vinawaathiri raia Iraq

14 Julai 2015

Umoja wa Mataifa umesema raia wa kawaida wanaendelea kuwa shabaha kuu ya mapigano nchini Iraq, wakati serikali ya nchi hiyo ikitangaza operesheni kubwa kulifursha kundi la dola la Kiislamu mkoani Anbar.

https://p.dw.com/p/1FyCb
Irak Offensive gegen IS-Terrormiliz in Anbar
Picha: Reuters/Str

Kwa mujibu wa ripoti ya kila mwaka kuhusu ulinzi wa raia, vurugu nyingi zaidi zimefanywa na kundi la Dola la Kiislamu IS, lakini pia wanachunguza za madai ya ukiukaji wa vikosi vya serikali na makundi washirika, ikiwemo kushindwa kuwalinda raia wakati wa mashambulizi ya angani na ardhini.

Ripoti hiyo imesema ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq ulirikodi vifo vya raia wasiopungua 3,345 waliouawa, na wasiopungua 7,423 waliojeruhiwa katika mapigano kuanzia Desemba 2014 hadi mwishoni mwa April mwaka huu. Wahanga wengi walikuwa wa mkoa wa Baghdad, wakifuatiwa na mikoa ya Anbar na Diyala.

Makundi ya silaha yenye mafungano au yanayoisaidia serikali pia yamefanya mauaji ya kulenga, yakiwemo ya wapiganaji waliotekwa kutoka IS na makundi washirika, kuwateka nyara raia, na kuharibu mali, imeongeza ripoti hiyo. Imesema katika kipindi cha miezi 16 zaidi ya raia milioni 2.8 wameyakimbia makaazi yao na wanaendelea kuwa wakimbizi ndani ya nchi yao, wakihusisha watoto milioni 1.3.

Wapiganaji wa IS.
Wapiganaji wa IS.Picha: picture-alliance/AP Photo

Kampeni ya kuikomboa Anbar yaanza

Wakati huo huo wanajeshi wa Iraq wakisaidiwa na wanamgambo jana walianzisha operesheni za kuukomboa mkoa mkubwa zaidi wa Anbar kutoka kwa wapiganaji wa IS, ikiwa ni miezi miwili tangu wapiganaji hao wauteke mji mkuu wa mkoa huo Ramadi na kutanua udhibiti wao.

Msemaji wa operesheni za pamoja alisema kampeni hiyo iliyoanza alfajiri, inawahusisha wanamgabo wa kishia wa kundi la Hashid Shaabi, vikosi maalumu, polisi na wapiganaji wa ndani wa makabila Wa Kisunni. Duru za kijeshi mkaoni Anbar zilisema walikumbana na upinzani mkali kutoka kwa IS ambao waliuwa wanajeshi 81 pamoja na wanamgambo wanaopigana upande wao.

Muungano unaoongozwa na Marekani umekuwa ukiswashambulia IS kwa mabomu nchini kote Iraq,na kuvisaidia vikosi vya ardhini vya Iraq na jeshi lake la angani lisilo na zana za kutosha. Siku ya Jumapili, muungano huo uliongeza mashambulizi karibu na mji wa Ramadi, ambapo mashambulizi 29 kati ya 39 yanayowalenga IS yalifanyika karibu na mji huo.

Jana Jumatatu, awamu ya kwanza ya ndege za kivita aina ya F-16 zilitua kwenye uwanja wa kijeshi wa Balad kaskazini mwa Baghad na kamanda wa jeshi angani la Iraq Luteni Jenerali Anwar Hama Amini alisema zitajiunga na operesheni mkaoni Anbar katika chache zijazo.

Iraq iliagiza ndege 36 za F-16 kutoka Marekani, lakini zimecheweleshwa kuwasilishwa kutokana na wasiwasi wa kiusalama, baada ya wapiganaji wa IS kuteka maeneo makubwa ya nchi hiyo mwaka uliyopita.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape,rtre.

Mhariri: Hamidou Oummilkheir.