1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

UN: Nusu ya wakaazi wa Gaza wanakabiliwa na baa la njaa

18 Machi 2024

Mkuu wa shirika la afya duniani WHO ameeleza wasiwasi wake juu ya hatma ya wagonjwa na raia wa Palestina baada ya jeshi la Israel kuanzisha oparesheni dhidi ya hospitali kubwa zaidi ya Ukanda wa Gaza ya Al-Shifa.

https://p.dw.com/p/4dryF
Gaza City Gaza Stadt | Flucht nach Aufruf, das Schifa-Krankenhaus & Umgebung zu verlassen
Picha: Dawoud Abo Alkas/Anadolu Agency/picture alliance

Oparesheni hiyo inafanywa huku ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo ikitahadharisha kuwa nusu ya wakaazi wa ukanda wa Gaza wanakabiliwa na baa la njaa na hali hiyo huenda ikageuka kuwa janga kubwa kufikia mwezi Mei.

Mkurugenzi wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba ana wasiwasi kuhusu hali katika hospitali ya Al-Shifa iliyoko kaskazini mwa Gaza.

Ghebreyesus amesema hospitali hazifai kutumiwa kama uwanja wa vita. Tahadhari hiyo ameitoa baada ya vikosi vya Israel kuivamia hospitali ya Al-Shifa kutokana na kile kilichoelezwa kuwa, ripoti za ujasusi za Israel zimesema hospitali hiyo inatumiwa na wanamgambo wa Hamas kuendesha shughuli zao.

Wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas imesema wakaazi karibu na hospitali hiyo wameripoti majeruhi kadhaa ambao hawakuweza kupata msaada wa haraka kutokana na mashambulizi ya risasi na makombora.

Soma pia:  Israel yafanya opereshi kwenye hospitali ya Al-Shifa Gaza

Ofisi ya idara ya habari ya Hamas imelaani mashambulizi ya Israel katika hospitali ya Al-Shifa na kuyaita mashambulizi hayo kuwa "uhalifu wa kivita.” Ofisi hiyo imeendelea kueleza kuwa, maelfu ya Wapalestina walikuwa wamekimbilia hospitalini humo kutafuta hifadhi.

Tedros ameweka wazi kwamba ni hivi karibuni tu ndio hospitali hiyo ya Al-Shifa imeanza tena kutoa huduma za matibabu japo kwa uchache.

Licha ya hospitali kulindwa na sheria ya kimataifa ya kibinadamu, taasisi hizo za kuhudumia wagonjwa zimelengwa mara kwa mara na mashambulizi ya Israel tangu kulipozuka vita kati ya Israel na Hamas Oktoba 7.

Umm Omar al-Mash'harawi, mmoja wa wakaazi wa Gaza amesema,  "Hakuna kitu cha kula wala kunywa. Watoto wanakufa. Watu wanakufa wakati ndege zinaangusha misaada.

Mkuu wa UNRWA azuiwa kuingia Gaza

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Palestina UNRWA Philippe Lazzarini
Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Palestina UNRWA Philippe LazzariniPicha: Mostafa Alkharouf/Anadolu/picture alliance

Wakati hayo yanaarifiwa, mamlaka ya Israel imemnyima ruhusa mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Palestina UNRWA ya kuingia ukanda wa Gaza.

Hayo yamesemwa na shirika hilo la UNRWA na waziri wa mambo ya nje wa Misri waliotaja zuio hilo kama hatua ya kushangaza na ambayo huko nyuma haijawahi kutokea.

Soma pia:  Netanyahu aapa kuendelea na vita licha ya shinikizo la kimataifa

Mkuu wa UNRWA Philippe Lazzarini, akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Cairo akiwa pamoja na waziri wa mambo ya nje wa Misri Sameh Shoukry, amesema alikuwa amekusudia kuelekea Rafah leo japo amezuiwa.

Kuzuiwa kwa Lazzarini kunatokea katikati ya mzozo mkubwa wa kibinadamu ukanda wa Gaza.

Hospitali katika Ukanda wa Gaza zaelemewa

Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo imetahadharisha kuwa nusu ya wakaazi wa ukanda huo wanakabiliwa na baa la njaa na hali hiyo huenda ikageuka na kuwa janga kubwa zaidi kufikia mwezi Mei iwapo hakutofanyika juhudi za kupeleka misaada.

Mkuu wa shirika la mpango wa chakula dunia WFP Cindy McCain amesema kuwa, wakaazi wa Gaza wanakufa kwa njaa sasa hivi.

Soma pia: WHO yalaani shambulio la Israel dhidi ya hospitali Gaza 

Ameongeza kuwa, baa hilo la njaa na utapiamlo uliosababishwa na binadamu unaenea kwa kasi.

WFP imesema takriban watu milioni 1.1 wanakabiliwa na baa la njaa.

Hali inaelezwa kuwa mbaya zaidi kaskazini mwa Gaza ambapo mashirika ya misaada yameeleza ugumu wa kusambaza vyakula na misaada mengine ya kibinadamu.