UN yalaani mashambulizi dhidi ya hospitali Kunduz
4 Oktoba 2015Mkuu wa Kamisheni ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa, Zeid Ra'ad al-Hussein, ametaka kufanyike uchunguzi kamili na ulio wazi kwa mashambulizi hayo ya usiku wa Jumamosi (Oktoba 2), akiongeza kwamba "ikiwa itathibitika mahakamani kuwa lilikuwa jambo la makusudi, basi mashambulizi haya yatakuwa sawa na uhalifu wa kivita."
Hospitali hiyo inayoendeshwa na Shirika la Madaktari Wasio Mipaka (MSF) ilikuwa muhimu sana kwenye mji wa Kunduz, ambao kwa siku kadhaa sasa umekuwa mikononi mwa wanamgambo wa Taliban. MSF inasema dalili zote zinaonesha kuwa mashambulizi hayo yalifanywa na ndege za Marekani.
Taarifa iliyotolewa na MSF inasema mnamo majira ya saa 8:10 usiku wa Jumamosi, hospitali hiyo ilishambuliwa mara kadhaa kwa mabomu na kuharibiwa vibaya, ambapo "wafanyakazi 12 na wagonjwa saba, watatu kati yao wakiwa watoto, waliuawa; watu 37 wakajeruhiwa."
Shirika hilo, ambalo ni maarufu kwa huduma zake za kiutu kwenye maeneo ya migogoro duniani, lilisema kwenye taarifa yake kwamba mashambulizi hayo "yanakiuka sheria za kiutu za kimataifa", kwani pande zote zilizo kwenye mapambano zilikuwa zimefahamishwa rasmi lilipo jengo hilo.
Marekani kufanya uchunguzi
Tayari Marekani imeahidi kufanya "uchunguzi kamili" juu ya mkasa huo. Mara tu baada ya taarifa za mashambulizi hayo kusambaa, Rais Barrack Obama alituma salamu zake za rambirambi kwa ndugu na jamaa wa wahanga, akiliita tukio hilo kuwa ni "janga".
Katika taarifa yake iliyotolewa na ikulu ya Marekani, Obama alibainisha kuwa wizara ya ulinzi imeanzisha uchunguzi juu ya tukio hilo, huku akisema watasubiri matokeo ya uchunguzi huo kabla ya kutoa tamko lolote.
Waziri wake wa ulinzi, Ashton Carter, alikiri kwamba vikosi vya kijeshi vya Marekani vilikuwa vinaendesha operesheni yao karibu na ilipo hospitali hiyo vikishirikiana na vile vya serikali ya Afghanistan, ingawa alisema pia wanamgambo wa Taliban nao pia walikuwepo.
Kwa mujibu wa mashahidi, mashambulizi hayo ya anga yalilenga jengo kuu la hospitali hiyo, ambalo lina vyumba vya kuhudumia wagonjwa mahututi na wa dharura, huku ikiyawacha majengo mengine yanayolizunguka.
Afghanistan yadai magaidi waliitumia hospitali
Wizara ya ulinzi ya Afghanistan ilielezea masikitiko yake kwa mashambulizi hayo, lakini ikasema "kundi la magaidi wenye silaha walikuwa wakilitumia jengo la hospitali hiyo kuwashambulia wanajeshi na raia."
MSF inasema wagonjwa wapatao 150 na wahudumu wao na pia wafanyakazi 80 wa shirika hilo walikuwemo kwenye hospitali hiyo wakati ikishambuliwa.
Jumuiya ya Kujihami ya NATO ilisema huenda wanajeshi wa Marekani wamehusika na mashambulizi hayo dhidi ya hospitali ambayo kwa muda mrefu ilikuwa ikiwatibu majeruhi wa pande zote za vita vinavyoendelea kwenye mkoa wa kaskazini wa Afghanistan.
"Mashambulizi haya ya anga yanaweza kuwa yamesababisha madhara yasiyokusudiwa karibu na jengo la hospitali. Uchunguzi unafanyika," ilisema taarifa ya NATO.
Tukio hili limeibua upya mashaka juu ya mashambulizi ya anga ya Marekani nchini Afghanistan, suala ambalo limekuwa tete sana kwenye vita vyake vya miaka 14 dhidi ya wanamgambo wa Taliban.
Mashambulizi haya yalifanyika baada ya wanamgambo hao kuuchukuwa mji huo wa kaskazini mwa Afghanistan siku ya Jumatatu (Septemba 28), ukiwa mji wa kwanza mkubwa kuchukuliwa na wanamgambo hao tangu mwaka 2001.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/dpa
Mhariri: Amina Abubakar