UN, Marekani zawataka Wahouthi kusitisha mashambulizi Marib
17 Februari 2021Wahouthi wanaoungwa mkono na Iran walianzisha tena mashambulizi yenye lengo la kuuteka mji wenye utajiri wa mafatu wa Marib ulioko umbali wa kilomita 120 mashariki mwa mji mkuu, Sanaa unaoshikiliwa na waasi hao.
Soma pia:Wahouthi washambulia viwanja vya ndege vya Saudi Arabia
Kuanguka kwa mji huo litakuwa pigo kubwa kwa serikali ya Yemen, inayoungwa mkono na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia, lakini pia kunatishia kusababisha janga kwa raia, wakiwemo mamia kwa maelfu ya watu walioachwa bila makazi wanaohifadhiwa katika makambi yaliyotelekezwa mjini humo.
Akielezea kustushwa na kuongezeka kwa mzozo mjini Marib, naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anaseshughulikia masuala ya kibinadamu Mark Lowcock, amesema mashambulizi dhidi ya mji huo yatawaweka hatarini raia milioni mbili, ambapo mamia kwa maelfu wanakabiliwa na uwezekano ya kulaazimika kukimbia.
Shinikizo la kidiplomasia?
Tim Lenderking, mjumbe mpya wa Marekani nchini Yemen aliyeteuliwa na rais Joe Biden kama sehemu ya juhudi za kumaliza vita nchini humo, amewahimiza Wahouthi kusitisha mashambulizi yao.
Lenderking aliwaambia waandishi habari mjini Washington, baada ya ziara katika kanda hiyo, kwamba mashambulizi hayo yanaweza kusababisha ugumu zaidi kwenye miundombinu ya kibinadamu ambayo tayari imeelemewa.
"Hatua juu ya Marib siyo mpya. Ni jambo ambalo Wahouthi wamekuwa wakilifikiria kwa muda wa miaka miwili iliyopita. Na iwapo hilo ni kijiweka katika nafasi bora kuelekea majadiliano au nini hasa lengo lao, siwezi kusema," alisema Lenderking.
"Tuna njia za kuwafikishia ujumbe Wahouthi na tunazitumia njia hizo kwa nguvu, kupitia mawasiliano ya moja kwa moja na uongozi wa mataifa muhimu yanayoshiriki."
Soma pia:Miaka 10 tangu vuguvugu la maandamano nchini Yemen
Ripoti za mamia ya vifo pande zote
Maafisa wa kijeshi wanaoiunga mkono serikali waliliambia shirika la habari la AFP kwamba waasi wamesonga mbele kuelekea mji huo kupitia maeneo mawili usiku, baada ya mapigano makali na vikosi vya serikali.
Maafisa hao wamesema wapiganaji kadhaa wameuawa kwa pande zote katika muda wa masaa 24 tu. Idadi jumla ya vifo kutokana na vita vya Marib haijulikani, lakini kuna ripoti zinazozungumzia kuuawa kwa mamia.
Soma pia:Yemen Kusini yachafuka baada ya jaribio la uhuru
Hadi mwanzoni mwa 2020, mji wa Marib ulikuwa umeepuka hali mbaya kabisa ya mzozo huo wa miaka sita, na uligeuka kimbilio la wengi.
Lakini utulivu huo wa kiasi ulitoweka kufuatia kuongezeka kwa mapigano mwaka uliyopita, na licha ya utulivu kujerea kwa muda mfupi kuanzia Oktoba, hofu inaongezeka juu ya janga jengine la kibinadamu.
Chanzo: Mashirika