UN kufikia maeneo zaidi Raqqa
12 Julai 2017Majeshi yanayoungwa mkono na Marekani yanakabiliana na kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS, katika eneo hilo walilolitangaza kuwa ni ngome yao.
Hatua hiyo mpya ya kupitisha vyakula imetoa mwanya kwa mpango wa chakula duniani WFP kufikisha chakula katika maeneo ya vijijini, Kaskazini mwa mji huo wa Raqqa kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mitatu. Shirika hilo la Umoja wa Mataifa hivi sasa linaweza kupeleka chakula kila mwezi kwa karibu watu 200,000 waliopo maeneo ambayo ni vigumu kufikika, pamoja na maeneo mengine jirani.
Kabla ya kufunguliwa upya kwa njia za ardhini zinazounganisha mji wa Aleppo, uliopo Magharibi na Hasakeh uliopo Mashariki, WFP ilitegemea zaidi njia ya anga kufikisha chakula.
"Njia hii ya ardhini kuchukua nafasi ya anga katika mchakato wa kufikisha chakula itasaidia kunusuru kiasi cha fedha kinachokadiriwa kufikia Dola Milioni 19 kwa mwaka, kwa kuwa kila lori linabeba wastani sawa na ule uliokuwa ukibebwa na ndege, lakini kwa gharama ya chini zaidi" amesema Jacob Kern mwakilishi wa WFP nchini Syria.
"Kwa gharama hizi na kuboreshwa kwa uwezekano wa kufikia maeneo hayo, hivi sasa tunaweza kuzifikia familia nyingi zaidi na watu wanaorejea nyumbani kwao, ambao wanahitaji msaada wetu wa kupatiwa chakula kila wakati", amesema.
Eneo moja ambalo linafikika kwa sasa ni mji wa Tabqa, ambao ulikombolewa kutoka mikononi mwa IS na majeshi Syria yanayoungwa mkono na Marekani mnamo mwezi May. WFP imesema, ilifanikiwa kuongeza kwa mara mbili idadi ya watu ambayo inawafikia, ambao wengi wao wamerejea makwao na hivi sasa wanajijenga upya kimaisha.
Harakati za kuukomboa mji wa Raqqa zilianza mwaka jana, kwa majeshi ya Syria kupambana kuwafurusha wapiganaji wa IS katika maeneo ya mji wa Raqqa, yakisaidiwa kwa na muungano wa kimataifa wa majeshi uliofanya mashambulizi ya angani.
Mwandishi: Lilian Mtono/APE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman