Kenya ilisaidia kumteka mkosoaji wa serikali ya Sudan Kusini
5 Oktoba 2023Hayo ni kulingana na uchunguzi ulioungwa mkono na Umoja wa Mataifa ambao umechapishwa hii leo Alhamisi.
Tume ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu nchini Sudan Kusini imesema mkosoaji huyo wa serikali Morris Mabior alitoweka baada ya kurejeshwa kwa nguvu nchini Sudan Kusini mwezi Februari na kuzuiliwa na Idara ya Usalama wa Taifa (NSS).
Tume hiyo ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema kutoweka kwa Mabior kumewatisha wakosoaji wengine wanaoishi nje ya Sudan Kusini na imelaumu nia ya serikali ya kuwafuata wapinzani nje ya mipaka yake.
Tume hiyo imesema pana haja ya kuwepo dhamira kwa majirani wote wa Sudan Kusini ya kuheshimu wajibu wao wa kisheria, hasa kutowarudisha watu ambao kwa hakika watakabiliwa na ukatili.
Msemaji wa polisi nchini Kenya ameliiambia shirika la habari la AFP kuwa hajaiona ripoti hiyo na hivyo hawezi kuzungumzia juu yake.