1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umri wa kuishi waongezeka kwa wanawake na wanaume

22 Februari 2017

Utafiti mpya umebaini watu wataendelea kuishi umri mrefu zaidi katika nchi zinazoendelea. Katika nchi hizo watu watafikisha umri wa miaka 90 na zaidi. Tofauti ya kuishi kati ya wanaume na wanawake pia imepungua

https://p.dw.com/p/2Y2AY
Iran alte Menschen Rente
Picha: Tamin

Watafiti kwa muda mrefu wamekuwa na mashaka mashaka iwapo kweli watu wanaweza kuishi kwa umri mrefu wa zaidi ya miaka 90 lakini wanasayansi wa chuo cha Imperial cha mjini London wamebainisha rasmi kuwa kwa sasa kuna uwezekano mkubwa kwa watu kuendelea kuishi zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali.

kwa mujibu wa Profesa Majid Ezzati, kufikia mwaka 2030 nchi kama Korea ya Kusini, Australia na uswizi miongoni mwa nchi nyingine zitajivunia kuwa watu wake wanaishi maisha marefu.  Korea ya Kusini ndio nchi ya kwanza duniani ambapo wanawake wa nchi hiyo wana matumaini ya kuishi na umri mrefu wa zaidi ya miaka 90 huku nchi nyingine zilizoendelea zikifuata kwa ukaribu kwa raia wake kuweza kuishi hadi kufikia miaka 88.

Profesa Ezzati hata hivyo anazishauri nchi husika kuanza kuweka mikakati kabambe ya kuwatunza vizee, amesema pia mabadiliko kama hayo yanahitaji mipango mingine pia ibadilike ili kuweka mambo sawa ametolea mfano mpango wa mafao ya uzeeni au pensheni.

Infografik Lebenserwartung von Menschen zum Zeitpunkt der Geburt ENG
Vipimo vya uhai katika nchi mbalimbali

Wanasayansi hao walizingatia vipengele mbalimbali katika utafiti wao juu ya  hali ya binadamu na jinsi anavyozeeka na kwa kiwango gani. Wanasayaansi hao wa chuo cha Imperial cha mjini London wamesema matibabu mazuri, uwezekano mkubwa wa kupata maji safi, lishe bora na kupungua kwa maradhi ya hatari ni mambo yanayochangia kwa kiwango kikubwa katika kuongezeka umri wa kuishi ikiwa ni pamoja na kuepuka vita, majanga asilia, njaa na magonjwa ya mripuko.  Wanasayansi hao wamesema sababu nyingine kama simanzi, shinikizo, umasikini, mfumo wa maisha pamoja na kufanya mazoezi ni mambo yanayochangia zaidi katika kupatikana jawabu iwapo watu wa eneo fulani wanaweza kuishi kwa umri mrefu zaidi au la.

Mnamo mwaka 2015 utafiti kama huo ulibaini nchi tano ambazo raia wake wangekuwa na umri mfupi zaidi wa kuishi ukiwa ni kati ya miaka 50 hadi chini ya miaka 55 kwa wanawake na wanaume zilikuwa ni nchi za barani Afrika.

Ripoti hiyo imeionyesha Marekani ikiburuza mkia katika nchi zilizo na utajiri mkubwa duniani. Watafiti wanasema kutokana hali inayoongezeka ya vifo vya watoto, mauaji na magonjwa sugu ni mambo yanachochea kupunguza umri wa kuishi.  Wataalamu hao wamesema vifo vingi vya watoto hutokea baada kuzaliwa nchini Marekani kuliko nchi nyingine yoyote yenye kiwango cha juu cha mapato, wanahofia kuwa hali hiyo itaendelea.
 
Mwandishi: Zainab Aziz/AFPE/ http://dw.com/p/2Y13P 

Mhariri: Yusuf Saumu