1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Waarabu kuunda jeshi la pamoja

29 Machi 2015

Viongozi wa mataifa ya Kiarabu wamekubaliana katika mkutano wa kilele (Jumapili 29.03.2015) nchini Misri kuunda kikosi cha kijeshi cha pamoja kukabiliana na vitisho vinavyoongezeka katika kanda yao.

https://p.dw.com/p/1EzEi
Viongozi wa nchi za Kiarabu waliohudhuria mkutano wa kilele wa umoja huo Sharm el- Sheikh, Misri.
Viongozi wa nchi za Kiarabu waliohudhuria mkutano wa kilele wa umoja huo Sharm el- Sheikh, Misri.Picha: Reuters/Egyptian Presidency

Viongozi wa mataifa ya Kiarabu wamekubaliana katika mkutano wa kilele (Jumapili 29.03.2015) nchini Misri kuunda kikosi cha kijeshi cha pamoja kukabiliana na vitisho vinavyoongezeka katika kanda yao.

Kwa mujibu wa azimio lililopitishwa na viongozi wa nchi hizo wawakilishi wa nchi za Kiarabu watakutana katika kipindi cha mwezi mmoja kutathmini uundaji wa kikosi hicho na kuwasilisha mapendekezo yao kwa mawaziri wa ulinzi katika kipindi kisichozidi miezi minne.

Rais Abdel Fatah al- Sisi wa Misri ameuambia mkutano huo wa kilele uliofanyika katika mji wa kitalii wa Sharm el - Sheikh kwamba ili kubeba dhamana kuu kutokana na changamoto kubwa zinazoyakabili mataifa hayo ya Kiarabu na kutishia uwezo wao,viongozi wa Kiarabu wamekubali kimsingi kuundwa kwa kikosi hicho cha jeshi la pamoja.

Kabla ya mkutano huo Mkuu wa Umoja wa Waarabu Nabil al- Arabi amesema uamuzi huo umechukuliwa kwa kiasi kikubwa ukiwa umekusudia kupambana na wapiganaji wa jihadi ambao wameteka sehemu kuwa za ardhi nchini Iraq na Syria na pia kujipenyeza nchini Libya.

Kundi la Dola la Kiislam ni tishio

Al- Arabi ameuambia mkutano huo wa kilele Jumapili kwamba eneo hilo linatishiwa na kundi la uharibifu ambalo linatishia uwepo wa dini na makabila mbali mbali yakiishi kwa pamoja na kwa amani,moja kwa moja alikuwa akilikusudia kundi la wapiganaji wa jihadi wa Dola la Kiislamu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Waarabu Nabil al-Arabi (kushoto) na waziri wa Mambo ya nje wa Misri Sameh Shoukry (kulia) mjini Sharm el- Sheikh Misri (29.03.2015)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Waarabu Nabil al-Arabi (kushoto) na waziri wa Mambo ya nje wa Misri Sameh Shoukry (kulia) mjini Sharm el- Sheikh Misri (29.03.2015)Picha: El-Shahed/AFP/Getty Images

Amekaririwa akisema "kilicho muhimu leo ni kupitishwa kwa uamuzi huo muhimu kutokan na msukosuko unaoathiri ulimwengu wa nchi za Kiarabu."

Misri ilikuwa ikishinikiza kuundwa kwa kikosi cha kukabiliana na hali ya dharura kitakachoweza kupambana na wanamgambo kwa haraka na suala hilo likazidi kwa la dharura wiki hii baada ya Saudi Arabia na washirika wa nchi za Kiarabu kuanzisha mashambulizi dhidi ya waasi wa jamii ya Wahouthi nchini Yemen.

Arabi amesema mashambulizi hayo yataendelea hadi hapo Wahouthi watakapoondoka katika maeneo waliyoyateka na kusalimisha silaha zao.

Mashambulizi kuendelea Yemen

Nchi kadhaa za Kiarabu ikiwemo Misri zinashiriki kijeshi katika mashambulizi hayo ambayo Mfalme Salman wa Saudi Arabia amesema hapo Jumamosi kwamba yataendelea hadi hapo wananchi wa Yemen watakapohakikishiwa usalama wao.

Athari ya mashambulizi ya Saudi Arabia mjini Sanaa.
Athari ya mashambulizi ya Saudi Arabia mjini Sanaa.Picha: AFP/Getty Images/M. Huwais

Rais wa Yemen Abedrabbo Mansour Hadi mwanzoni mwa mkutano huo ametowa wito wa kukomeshwa kwa mashambulizi hayo pale tu Wahouthi watakaposalimu amri na kumwita kiongozi wa waasi hao wa Kihouthi kuwa kibaraka wa Iran.

Hata hivyo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki-moon amewataka viongozi hao wa Kiarabu kutafuta suluhisho la amani kwa mzozo huo wa Yemen.

Licha ya kuungwa mkono kwa uundaji wa kikosi hicho cha cha pamoja cha Waarabu bado itachukuwa miezi mingi kukiunda na baadae kufanya kazi kwa misingi rasmi.

Sisi amesema katika mahojiano ya hivi karibuni kwamba pendekezo la kuunda kikosi hicho cha pamoja limekaribishwa hususan na Jordan ambayo yumkini ikashiriki pamoja na Saudi Arabia,Umoja wa Falme za Kiarabu na Kuwait.

Nchi kuchangia kwa uwezo wake

Aaron Reese naibu mkurugenzi wa utafiti katika Taasisi ilioko Washington Marekani ya Masomo ya Vita amesema kila mmoja ya nchi hizo itachangia kwa uwezo tafauti ilio nao.

Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Waarabu mjini Sharm el -Sheikh,Misri.(29.03.2015)
Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Waarabu mjini Sharm el -Sheikh,Misri.(29.03.2015)Picha: El-Shahed/AFP/Getty Images

Wajordan wanajulikana kwa uwezo walio nao vikosi vyao maalum wakati Misri inatambulika kwa kuwa na jeshi kubwa na makambi karibu na Libya.

Misri ilikuwa ikitaka uungaji mkono wa Umoja wa Mataifa kuingilia kati nchini Libya na kutupilia mbali jaribio la mazungumzo ya amani kwa jirani yake huyo wa Afrika kaskazini kuwa hayafai.

Mchakato wa amani wa Israel na Wapalestina kama ilivyo katika kila mkutano wa kilele wa Umoja wa Waarabu pia ulitajwa kwenye agenda na masuala mengine yaliyopewa pia kipau mbele ni kujiingiza kwa Kundi la Dola la Kiislamu nchini Iraq na Syria na mzozo wa Libya.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri : Sudi Mnette