1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya watoa ahadi mpya kuhusiana na haki za binadamu.

Sekione Kitojo15 Novemba 2007

Ripoti mpya ya umoja wa Ulaya juu ya jinsi inavyoshughulikia suala la haki za binadamu inasema kuwa kundi hilo la mataifa 27, linadhamira ya kupambana kuelekea kuzuwia uhalifu wa kimataifa na kukomesha hali ya kuepuka adhabu kwa wale wanaohusika na matendo ya uhalifu

https://p.dw.com/p/CH6s

.

Kwa mujibu wa wanaharakati , wanaofanya kampeni , dhamira hiyo haijaonekana katika kujibu madai ya mauaji ya halaiki katika jimbo la Darfur. Mwezi Aprili , mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa vita ICC, ilitoa hati ya kukamatwa kwa Ahmed Haroun , waziri wa masuala ya kiutu wa Sudan na Ali Kosheib , mtu mashuhuri katika kundi la kihalifu la Janjaweed ambao wanatuhumiwa kufanya mauaji makubwa wakiungwa mkono na serikali mjini Khartoum.

Watu hao wawili wanakabiliwa na mashtaka 51 ya uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita, ikiwa ni pamoja na mauaji, ubakaji, kuwalazimisha watu kukimbia makaazi yao na mateso.

Ripoti ya haki za binadamu ya umoja wa Ulaya inadokeza kuwa imeteua hivi karibuni mjumbe maalum kushughulikia mzozo wa Darfur, ambao umesababisha vifo vya watu wapatao 200,000 na kuwalazimisha wengine milioni 2.5 kukimbia makaazi yao katika muda wa miaka minne na nsu ya mzozo huo. Ripoti hiyo imeongeza kuwa mwanadiplomasia kutoka Denmark Torben Brylle amepewa madaraka ambayo ni pamoja na jukumu la kupambana dhidi ya wahusika kuepuka kuadhibiwa. Lakini tangu pale mahakama ya kimataifa kutoa hati za kukamatwa watuhumiwa, Ahmed Haroun ameteuliwa kuwa mwenyekiti wa kamati inayohusika na usalama nchini Sudan , ikiwa ni pamoja na jimbo la magharibi nchini humo la Darfur. Kama sehemu ya majukumu yake , anaweza kutathmini malalamiko ya kuendewa kinyume haki za binadamu katika jimbo la Darfur. Lotte Leicht , mkurugenzi wa Human Rights Watch mjini Brussels , amesema kuwa kwa kweli haiwezi kuelezeka , kwa vipi serikali za umoja wa Ulaya zimeweza kujibu kuteuliwa kwa Haroun katika wadhifa wake mpya kwa kukaa kimya kabisa.

Leicht anawataka mawaziri wa mambo ya kigeni wa umoja wa Ulaya wanaokutana wiki ijayo Novemba 19 – 20 kuionya rasmi Sudan kuwa wataiwekea vikwazo serikali ya nchi hiyo, iwapo itaendelea kuupuzia hati hizo za kukamatwa dhidi ya Kosheib na Haroun. Hatua kama hizo zimechukuliwa hivi karibuni dhidi ya Uzbekistan. Maafisa wanane wa Uzbekistan walipigwa mafuruku kusafiri kwenda katika mataifa ya Ulaya Oktoba 2005, kujibu kukataa kwa nchi hiyo kuruhusu kufanyika kwa uchunguzi wa kimataifa kuhusiana na mauaji ya Andijan Mei 2005, ambapo majeshi ya Uzbekistan yaliwauwa waandamanaji ambao hawakuwa na silaha. Licha ya kuwa hatua ndogo zimeonekana kuhusiana na haki za binadamu, umoja wa Ulaya ulikubali kusitisha vikwazo hivyo mwezi uliopita , lakini umeonya kuwa vinaweza kurejeshwa iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa na Uzbekistan. Licha ya hali mbaya ya kiutu inayosababishwa na hali katika jimbo la Darfur , maafisa nchini Ureno, nchi ambayo hivi sasa inashikilia urais wa umoja wa Ulaya , wamethibitisha kuwa suala hilo halitakuwa katika ajenda ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya kigeni wiki ijayo.