Umoja wa Ulaya watangaza mpango wa kugawa waomba hifadhi
23 Septemba 2020Mkataba huo mpya kuhusu wahamiaji na waomba hifadhi uliwasilishwa na kamishna wa umoja huo anayehusika na masuala ya ndani Ylva Johansson na makamu wa kamishna Margaritis Schinas.
Johansson anataka mataifa 27 wanachama kuweka nia ya kugawana mzigo wa kushughulikia maombi ya wahamiaji wanaowasili katika mataifa hayo. Ni dhahiri kwa kila mtu kwamba mshikamano wa muda ama mshikamano wa kujitolea hautoshi. Hii imethibika kwa miaka mingi sasa, amesema, na kusisitiza kuwa sasa itabidi kuwa lazima. Mpango huo utalazimisha kuonesha mshikamano na mataifa yote ya Umoja wa Ulaya kwa mataifa yaliyo mstari wa mbele kama Ugiriki, Italia na Malta.
Mpango huo umetangazwa wiki mbili baada ya moto uliozuka na kuharibu kabisa kambi ya wakimbizi ya Moria, Halmashauri ya Umoja wa Ulaya imesema inataka kuweka kituo cha kuwapokea wahamiaji katika kisiwa cha Ugiriki cha Lesbos kitakachoendeshwa kwa pamoja na Ugiriki.
Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen alitangaza kuundwa kwa kikosi kazi kipya, ambacho, kwa msaada wa mashirika ya Umoja wa Ulaya, kitasaidia kuweka hali bora ya mazingira kwa watu katika kisiwa hicho kwa njia imara zaidi.
Kambi ya Moria katika kisiwa cha Ugiriki cha Lesbos, ambayo iliwahifadhi karibu wahamiaji 12,000, kiliungua moto kiasi ya wiki mbili zilizopita. Watu karibu 10,000 walihamishiwa katika eneo la muda la mahema.