1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya watafuta njia ya kuisadia Libya

Mjahida18 Aprili 2016

Mwaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wanatafuta njia za kuisaidia serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya, na pia kujadili namna ya kudhibiti uhamiaji haramu kutoka taifa hilo la Kaskazini mwa Afrika.

https://p.dw.com/p/1IXuL
London Außenminister Philip Hammond Downing Street in London
Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Philip HammondPicha: Getty Images/C. Ratcliffe

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Philip Hammond ndiye afisa wa hivi karibuni wa Umoja wa Ulaya, kuzuru Libya hii leo baada ya wenzake kutoka Ujerumani na Ufaransa kufika nchini humo mwishoni mwa juma katika juhudi za kuunga mkono utawala wa Waziri Mkuu mteule Fayez Serraj.

Hammond alipelekwa chini ya ulinzi mkali hadi katika kambi ya kijeshi, ambako utawala wa Waziri Mkuu Fayez Serraj unajaribu kujiimarisha. Waziri Hammond amesema nchi yake inaunga mkono mikakati ya kurejesha amani na uthabiti katika taifa zima la Libya, huku akitangaza dola milioni 14 za kuisaidia serikali mpya kuimarisha taasisi za kisiasa, uchumi, usalama na haki.

Uingereza kutoa mafunzo kwa vikosi vya Libya iwapo msaada huo utahitajika

Mataifa ya Magharibi yanatumai kuwa serikali mpya ya Libya itawaunganisha walibya wote na kuisaidia nchi hiyo kupambana na wanamgambo wa dola la kiislamu, IS. Aidha maafisa wa Uingereza wamesema nchi hiyo iko tayari kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa Libya juu ya namna ya kukabiliana na kundi hilo lililo na itikadi kali. Hata hivyo maafisa hao hawakuweka wazi taarifa kwamba kuna njama ya maelfu ya wanajeshi wa Magharibi kupelekwa nchini Libya, hivi karibuni.

Libyen Tripolis Fayez Serraj Einheitsregierung
Waziri Mkuu wa Libya Fayez SerrajPicha: Getty Images/AFP/Str

Kwa upande wake waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa, Jean-Marc Ayrault, amesema serikali mpya inapaswa kuanza kufanya kazi vizuri na kwamba ni jukumu la Umoja wa Ulaya kuipa serikali hiyo kila nafasi ya kuweza kufanikiwa.

Mawaziri hao wa mambo ya nje kutoka mataifa 28 ya Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kuwa na mazungumzo kwa njia ya simu na Waziri Mkuu mteule Serraj baadaye hii leo jioni.

Libya ilitumbukia katika mapigano baada ya kuuwawa kiongozi wake Muammar Gadhafi mwaka wa 2011, hali iliyotoa nafasi kwa dola la kiislamu kujiimarisha huku serikali mbili hasimu zikipigania uongozi, moja iliyoko mjini Tripoli inayoungwa mkono na wanamgambo na nyengine Mashariki mwa Libya inayotambuliwa Kimataifa.

Mwandishi: Amina Abubakar/AP/AFP

Mhariri: Josephat Charo