1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya wasisitiza udhibiti mkali zaidi wa bajeti

19 Novemba 2011

Halmashauri ya umoja wa Ulaya inataka udhibiti mkali zaidi wa bajeti za taifa ili kupambana na mzozo wa madeni wa eneo la euro, ameeleza afisa mwandamizi jana Ijumaa.

https://p.dw.com/p/13DUS
Rais wa halmashauri ya umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso, anahitaji udhibiti mkali zaidi wa bajeti za taifa.Picha: dapd

Halmashauri ya Umoja wa Ulaya inataka udhibiti mkali zaidi wa bajeti za taifa ili kupambana na mzozo wa madeni wa eneo la euro, amesema afisa mwandamizi jana Ijumaa , wakati mkuu wa Benki Kuu ya Umoja wa Ulaya amehimiza kuchukuliwa hatua za haraka kuhusiana na mfuko wa eneo la euro wa uokozi kwa mataifa yaliyo katika matatizo.

wakati mzozo huo unaelekea kuingia katika nchi ya tano ya eneo la euro mwishoni mwa juma hili, waziri mkuu mtarajiwa nchini Hispania ametoa wito kwa masoko ya fedha kutoa nafasi ya kupumua wakati akianza kupambana na matatizo ya nchi yake, kitu ambacho hatakipata.

Mjini Berlin, kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameweka wazi kuwa anapendelea mwelekeo wa hatua kwa hatua katika kupambana na mzozo huu ambao unasambaa hadi katika mataifa makubwa katikati ya mradi wa euro na kuzikumba nchi kama Italia, Hispania na huenda Ufaransa.

Deutschland EU Großbritannien David Cameron bei Angela Merkel in Berlin
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel (kulia ) akiwa na waziri mkuu wa Uingereza David Cameron mjini Berlin jana.Picha: dapd

Moja ya mambo ya msingi ya mtazamo wa Merkel ni kuweka mbinyo kwa yale mataifa wanachama wa eneo la euro ambayo yanakiuka utaratibu wa bajeti zao na kudhibiti matatizo hayo. Ushauri juu ya vipi hali hii inaweza kufanyika katika kipindi cha muda mfupi ulitoka katika halmashauri ya umoja wa Ulaya mjini Brussels. Maafisa waandamizi wa eneo la euro wamesema kuwa halmashauri ya umoja wa Ulaya itapendekeza wiki ijayo hatua kali za uangalizi wa uchumi wa mataifa pamoja na bajeti, hali ambayo inaweza hatimaye kusababisha aina fulani ya dhamana zinazopendelewa na uongozi wa kundi hilo kwa jumla.

Iwapo mpango huo utakubaliwa na viongozi wa umoja wa Ulaya , hatua ambayo huenda ikachukua mwaka mmoja au zaidi, mataifa wanachama huenda yakatoa sehemu kubwa ya mamlaka yake kuhusiana na utawala wa fedha kwa uongozi wa umoja wa ulaya mjini Brussels. Maafisa wa halmashauri ya umoja wa ulaya huenda hata wakaonekana katika mabunge ya kitaifa katika hatua ya kuhalalisha madai yao kuhusu bajeti.

Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre

Mhariri: Prema Martin