1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya warefusha vikwazo dhidi ya Zimbabwe

Mohamed Abdul-Rahman19 Februari 2007

Mugabe azidi kukosolewa kwa kukandamiza demokrasia na ukiukaji wa haki za binaadamu.

https://p.dw.com/p/CHJv
Rais Rober Mugabe wa Zimbabwe
Rais Rober Mugabe wa ZimbabwePicha: AP

Utawala wa Rais Robert Mugabe nchini Zimbabwe ,unazidi kulaumiwa vikali kwa ukandamizaji unaoendelea dhidi ya upinzani pamoja na ukiukaji wa haki za binaadamu nchini humo. Kutokana na hali hiyo Umoja wa ulaya umerefusha vikwazo dhidi ya Zimbabwe hadi Februari mwakani, 2008.

Umoja wa ulaya awali iliiwekea vikwazo Zimbabwe 2002, baada ya uchaguzi ambao upinzani unashikilia ulifanyiwa udanganyifu na Rais Mugabe anayetawala tangu 1980 kutangazwa mshindi.

Hatua ya Umoja wa ulaya kurefusha vikwazo hivyo kwa mwaka mmoja zaidi ilichukuliwa bila ya mjadala wowote,wakati wa kuanza mkutano wa mawaziri mjini Brussels jana, na inafuatia wito uliotolewa na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel wiki iliopita wakati akihutubia mkutano wa kilele kati ya Afrika na Ufaransa mjini Cannes. Merkel ambaye nchji yake ni mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa ulaya alisema,“Hapa sitaki kuficha kuwa tunaifuatilia hali nchini Zimbabwe tukiwa na wasi wasi mkubwa. Kuwatisha wapinzani, kuwatia uwoga wakulima na kubomoa mitaa wanakoishi masikini-haya yote si halali. Ndiyo maana ninaziomba nchi jirani na Zimbabwe zituunge mkono na kutumia ushawishi wao , ili kuwasaidia wale masikini”

Taarifa iliotolewa na Umoja wa ulaya kuhusu kuendelezwa vikwazo inapiga marufuku kusafiri katika nchi wanachama kwa yeyote aliyeshiriki katika hatua za kuhatarisha na kukandamiza demokrasia na haki za binaadamu, pamoja na kuzuiwa kwa mali zao.Hatua hiyo inawahusu maafisa wapatao 130 akiwemo Rais Mugabe mwenyewe, mawaziri wake wa sasa na wa zamani na viongozi wa chama tawala ,ZANU-PF.

Amri inayowapiga marufuku maafisa hao kusafiri katika nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, imezusha matatizo kwa Rais Mugabe mnamo miaka iliopita, na hasa palipohusika na mikutano ya Viongozi wakuu wa Umoja wa ulaya na Afrika. Baada ya mkutano wa kwanza kufanyika Cairo nchini Misri Aprili 2000, wa pili uliokua ufanyike mwezi huo mwaka 2003 ulicheleweshwa baada ya kuzuka mabishano baina ya nchi za kiafrika na ulaya, na hasa mtawala wa zamani- Uingereza, kuhusu amri inayompiga marufuku Rais Mugabe. Hivi sasa mkutano huo wa kilele umepangwa kufanywa baadae mwaka huu mjini Lisbon nchini Ureno.

Hatua mpya ya kurefusha vikwazo ina maana pia kwamba msaada wa maendeleo unaotolewa na Umoja huo kwa Zimbabwe unaendelea kusitishwa, isipokua tu msaada wa moja kwa moja unaotolewa kwa umma wa nchi hiyo.

Hatua hiyo iliotangazwa jana, imekuja katika wakati ambao chama kikuu cha upinzani Movement for Democratic Change –MDC kikila kiapo kuwa kitaendelea na maandalizi ya maandamano na mikutano kadhaa ya hadhara kupinga utawala wa Rais Mugabe, licha ya hatua ya matumizi ya nguvu iliochukuliwa na polisi mwishoni mwa juma lililopita, kuzuwia mkutano ulioitishwa na kiongozi mkuu wa chama hicho Morgan Tsvangirai mjini Harare.Polisi iliuvunja mkusanyiko huo, licha ya MDC kupata kibali cha mahakama kuu, kilichoipa haki ya kuandaa mkutano huo.

Uchaguzi ujao wa Rais unatarajiwa mwaka ujao, lakini Mugabe anayeitawala Zimbabwe kwa mwaka wa 27 sasa anajaribu kuuahirisha hadi 2010, ili ufanyike sambamba na uchaguzi wa bunge.