Umoja wa Ulaya wamshinikiza Mugabe kukubali matokeo
4 Aprili 2008Matokeo ya urais nchini Zimbabwe yaliyofanyika mwishoni mwa juma hadi sasa hayajulikani.Umoja wa Ulaya nao umeingia katika shinikizo la kutaka matokeo hayo kutolewa mara moja,huku yale yaliojiri kwenye mkutano wa dharura wa kamati kuu ya chama cha Bw Mugabe cha ZANU PF,ulioitishwa baada ya chama hicho kufanya vibaya katika uchaguzi hayajatolewa hadharani.
Serikali ya sasa ya Zimbabwe inayoongozwa na Bw Robert Mugabe ina kabiliwa na shinikizo moja baada ya lingine kila kukicha,tangu kufanyika kwa uchaguzi mkuu mwishoni mwa juma.
Umoja wa Ulaya umetoa shinikizo kadhaa kwa kiongozi wa chama cha ZANU PF,Robert Mugabe.Miongoni mwa shinikizo kadha ni lile la kumtaka kuheshimu matokeo ya uchaguzi mkuu wa urais.
Shinikizo la umoja huo linakuja kutokana na hofu kuwa huenda Mugabe anapanga njama za kubadili matokeo ya uchaguzi ili yampendelee yeye .Hayo yanachochewa na matamshi pamoja na matukio kadhaa.Kabla ya uchaguzi Mugabe mwenyewe alisema kuwa Zimbabwe kamwe haitakubali kubadili siasa kwa kushinikizwa na watu wa nje.
Mbali na hayo hadi kufikia sasa tume ya uchaguzi imeshindwa kutoa matokeo ya urais japo ilitoa ya viti vya ubunge ambapo upinzani ulijinyakulia viti vingi kuliko chama cha ZANU PF.
Hali hiyo imemlazimisha rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini ambae alipewa jukumu la kupatanisha nchini Zimbabwe kabla ya kufanyika uchaguzi,kutoa matamshi yanayosema kuwa wanategemea kila upande utaheshimu yatakayotolewa.
Aliekuwa waziri wa fedha katika serikali ya Bw Mugabe na mwanachama wa zamani wa ZANU PF na mgombea wa urais wa kujitegemea Simba Makoni amesema kuwa yuko tayari kushirikiana na Tsvangirai.Meneja wake nae akiwa mwanachama wa zamani wa ZANU PF, Ibbo Mandaza anasema kuwa hatua za kumbakiza madarakani Mugabe si za maana.
Kipigo cha mwishoni mwa juma kinaonekana ndio kikubwa kuwahi kuukumba utawala wa Mugabe uliodumu miaka 28. Chama hicho kimelazimisha kuitisha mkutano wa halmashauri kuu mjini Harare kupanga mikakati mingine ambayo haijajulikana baado.
Matokeo ya mkutano huo yakiwa yanasubiriwa kama yalivyo matokeo ya urais,umoja wa Ulaya pia umesema leo kuwa unachunguza habari kamili kuhusiana na kisa cha kukamatwa kwa waandishi wawili wa kigeni waliokamatwa na polisi mjini Harare.Msemaji wa Louis Michel wa Umoja wa Ulaya-John Clandy amesema kuwa wanaguswa na vitendo vya kukamatwa kwa waandishi wa habari ambao wanafanya kazi zao.
Wakuu nchini Zimbabwe wanasema kuwa waandishi hao walikamatwa kwa kuvunja sheria za nchi hiyo ambapo walifanya kazi bila kibali.
Waandishi hao mmoja analifanyia kazi gazeti la The New York Times na mwingine ni raia wa Uingereza. Hapo awali serikali iliwapiga marufuku waandishi wa habari wa nje kuripoti kuhusu uchaguzi kutoka Zimbabwe na ilikuwa imewaonya kuwa watamchukulia hatua kali yeyote atakaekamatwa akifanya kazi kinyume na sheria.
Kwa hali yoyote ile watu wa ndani na nje ya nchi hiyo wako chonjo wakisubiri kwa hamu matokeo ya mkutano na pia ya uchaguzi wa Urais.