Umoja wa Ulaya wakataa kuingilia suala la Catalonia
20 Oktoba 2017Rais wa baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk aliwaeleza waandishi wa habari wakati wa mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels kuwa suala la Catalonia haliko katika ajenda za mkutano huo.
" Sisi sote tuna mawazo yetu, hisia na tathimini zetu lakini kwa taarifa tu hakuna nafasi ya Umoja wa Ulaya kuingilia mgogoro huo na nchi wanachama wanaelewa fika kuwa hakuna nafasi hiyo". Alisema Tusk.
Hayo yanajiri mnamo wakati rais wa jimbo la Catalonia Carles Puigdemont akipuuza muda wa mwisho aliopewa na serikali ya mjini Madrid kubatilisha nia yake ya kutaka kutangaza uhuru wa jimbo hilo ambapo siku tatu alizopewa kufanya hivyo zimemalizika asubuhi ya leo na badala yake kiongozi huyo amemuandikia barua waziri mkuu Mariano Rajoy akitishia kutangaza uhuru wa jimbo la Catalonia.
"Puigdemont amesema " Iwapo serikali ya mjini Madrid itaendelea kukataa majadiliano pamoja na kuzima suala hili basi bunge la Catalonia litaendelea" alisema Puigdemont.
Rajoy anapanga kutumia ibara ya 155 ya katiba ya mwaka 1978 ambayo inamruhusu kuchukua mamlaka ya jimbo lolote iwapo itabainika limevunja sheria.
Kakao maalumu cha baraza la mawaziri kimepangwa kufanyika Jumamosi ili kuandaa orodha ya hatua kwa ajili ya kuidhinishwa na seneti
Serikali ya Uhispania yapanga kumpokonya madaraka Puigdemont
Hatua zinazofikiriwa ni pamoja na kumuondolea madaraka ya urais kiongozi wa jimbo la Catalonia Carles Puigdemont, kulipokonya jimbo hilo madaraka ya kusimamia masuala ya elimu na shule, kuitisha uchaguzi mpya, kuvunja bunge la jimbo hilo pamoja na kudhibiti vyombo vya habari vya umma vinavyoonekana kuwa njia inayotumiwa na jimbo hilo kutangaza nia yake ya kutafuta uhuru wa jimbo hilo.
Hadi sasa Puigdemont ametoa mwito wa kufanyika majadiliano kati ya uongozi wa jimbo hilo na serikali ya mjini Madrid pamoja na wapatanishi wa kimataifa.
Kwa upande wake Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akizungumzia suala hilo mjini Brussels amesema kuwa wanaunga mkono msimamo wa serikali ya Uhispania na kuongeza kuwa ana mataumaini suluhu itapatikana kwa kuzingatia katiba ya Uhispania huku Waziri Mkuu wa Uholanzi Mark Rutte akisema hilo ni suala la ndani kauli iliyoungwa mkono na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliyefanya kikao cha faragha na na Waziri Mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy pembezoni mwa mktano huo wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya.
Kwa mujibu wa mwanadiplomasia wa Ufaransa aliezungumza na shirika la habari la Reuters Macron alisema ana imani kubwa na Rajoy katika kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo wa kisiasa. Naye Rais wa Urusi Vladimir Putin alisema mgogoro wa Catalonia ni suala la ndani la Uhispania na kukosoa undumilakuwili wa nchi za magharibi kwa kuunga mkono suala la Kosovo na kujiweka kando katika masuala mengine kama hayo.
Wakazi wa Catalonia wapatao milioni 7.5 wamegawanyika kuhusiana na hoja hiyo ya kujitenga ambapo wapiga kura wengi wanaopinga uhuru wa wa jimbo hilo walijiweka kando na kura hiyo ya maoni ambayo ilitangazwa kuwa ni batili na mahakama ya kikatiba ya Uhispania.
Wakati huohuo viongozi wa Umoja wa Ulaya wanakutana mjini Brussels kujaribu kutafuta njia za kuharakisha mazungumzo yanayohusiana na mchakato wa Uingereza kujiondoa kwenye Umoja huo ujulikanao kama Brexit. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema hana mashaka yoyote na anaimani Umoja wa Ulaya na Uingereza watapata mafanikio katika suala hilo la Brexit.
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May amesema mazingira yanayowekwa na viongozi hao wa Umoja wa Ulaya kuhusiana na suala hilo yatasaidia kuwezesha kusonga mbele kwa mchakato huo wa Brexit.
Mwandishi: Isaac Gamba/dw/rtre/ape
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman