Umoja wa Ulaya waiondolea vikwazo Zimbabwe
17 Februari 2014Uamuzi huo wa kusitisha vikwazo vya kusafiri na kuzuiliwa mali dhidi ya watu wanane ni ishara ya wazi kutoka kwa mawaziri wa kilimo wa Umoja wa Ulaya, baada ya serikali za Umoja huo kukubaliana na mabadiliko hayo. Hata hivyo, Rais Mugabe na mkewe, Grace, wanaendelea kukabiliwa na vikwazo hivyo.
Umoja wa Ulaya uliweka vikwazo vikali dhidi ya Zimbabwe mnamo mwaka 2002, baada ya serikali ya Mugabe kuwahamisha kwa nguvu wakulima wa Kizungu kutoka kwenye ardhi za kilimo.
Hata hivyo, vikwazo hivyo vimekuwa vikipunguzwa mwaka hadi mwaka kufuatia maendeleo ya kisiasa, ingawa hatua ziliendelea kuchukuliwa dhidi ya Mugabe na wapambe wake.
Wiki iliyopita, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton, aliwaambia wabunge wa Bunge la Ulaya kwamba Zimbabwe inasonga mbele na Umoja huo unapaswa kuchukuwa hatua. "Ikiwa mambo yatakwenda vibaya, tutarudisha tena vikwazo," alisema Ashton.
Licha ya marufuku ya kusafiri kuendelea kumuandama Mugabe, bado kiongozi huyo mkongwe zaidi kusini mwa Afrika anaruhusiwa kuhudhuria mkutano wa kilele wa viongozi wa Afrika na Umoja wa Ulaya mwezi Aprili, mjini Brussels. Hii ni kwa sababu nchi za Ulaya hazilazimiki kuheshimu vikwazo vya Umoja wa Ulaya ikiwa zinafanya mikutano mikubwa ya kimataifa.
Vikwazo vya silaha vya Umoja wa Ulaya vitaendelea dhidi ya kiwanda cha kijeshi cha Zimbabwe. Marekebisho haya ya vikwazo yataanza kazi rasmi baada ya kuchapishwa kwenye gazeti rasmi la Umoja wa Ulaya.
Mugabe aachia huru wafungwa
Hatua hii ya Umoja wa Ulaya imesadifiana na uamuzi wa Rais Mugabe kuwaachia wafungwa 2,000 hivi leo, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
Chini ya msamaha huo, wanawake wote wameachiliwa huru, isipokuwa wale wanaotumikia vifungo vya maisha, lakini wafungwa wote walio chini ya miaka 18 wameachiwa huru, bila ya kujali makosa waliotiwa hatiani.
Msamaha huo unawahusu pia wafungwa wote wenye ugonjwa usiopona na wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 70. Hata hivyo, wafungwa waliotiwa hatiani kwa mauaji, uhaini, kubaka, utekaji nyara na wizi wa kutumia silaha na wale wanaotumikia vifungo vilivyotolewa na mahakama za kijeshi, hawafaidiki na msamaha huo.
Katiba ya Zimbabwe inamruhusu Rais kutoa msamaha kwa wafungwa wakati wowote anaoona inafaa. Zaidi ya wafungwa 100 walikufa mwaka jana nchini Zimbabwe kutokana na upungufu wa chakula, kwa mujibu wa makundi ya haki za binaadamu.
Kwa mujibu wa taarifa ya serikali, idadi ya wafungwa walioachiwa huru ni zaidi ya asilimia 10 ya wafungwa wote nchini huyo, ambao mwaka jana walikuwa 18,460. Jela za nchi hiyo zina uwezo wa kuchukuwa wafungwa 17,000.
Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/Reuters
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman