1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya una wasiwasi juu ya Ugiriki

8 Mei 2012

Baada ya chaguzi kufanyika nchini Ufaransa na Ugiriki, wasiwasi umetanda katika Umoja wa Ulaya kuhusu kuzuka kwa mgogoro mpya wa sarafu ya Euro. Hili linakuja wakati ambapo vyama vya Ugiriki vimeshindwa kuunda serikali.

https://p.dw.com/p/14rcw
Nembo ya sarafu ya euro
Nembo ya sarafu ya euroPicha: picture alliance/dpa

Kwa kawaida kamisheni ya Umoja wa Ulaya haitoi maoni yake juu ya matokeo ya uchaguzi. Lakini suala la Ugiriki ni tofauti kwani linahatarisha Umoja huo, kwa ujumla. Wagiriki wengi wamevipigia kura vyama vilivyo na mashaka juu ya hatua za kufunga mkaja au vyama vinavyopinga kabisa hatua hizo. Kwa hivyo, huenda serikali mpya ikazipuuza hatua za kubana matumizi zilizoidhinishwa na Umoja wa Ulaya. Msemaji wa Kamisheni ya Umoja huo, Bi Pia Ahrenkilde, ameonya: "Kamisheni inatarajia na kutumaini kwamba serikali mpya ya Ugiriki itayafuata makubaliano yaliyofikiwa."

Msemaji huyo ameongezea kusema kwamba Umoja wa Ulaya uko tayari kuendelea kuiunga mkono Ugiriki na unatarajia kwamba patakuwepo na hali ya uwajibikaji katika kuunda serikali mpya. Amadeu Altafaj, ambaye ni msemaji wa Kamishna wa fedha wa Umoja wa Ulaya alisisitiza: "Tunaweza kufanya mambo mengi kuisaidia Ugiriki na tunafanya hivyo," alisema Altafaj. "Nchi mwanachama na walipa kodi katika nchi zote zinazotumia sarafu ya Euro wanatoa mshikamano. Lakini mshikamano si jukumu la upande mmoja tu."

Wagiriki wakipiga kura
Wagiriki wakipiga kuraPicha: DW

Mpango kabambe wahitajika

Joseph Daul ni mwenyekiti wa chama cha kihafidhina cha Ugiriki katika bunge la Umoja wa Ulaya na ameelezea kwamba anahofia kuwa matokeo ya uchaguzi wa Ugiriki yanaweza kuifanya nchi hiyo ikajitoa katika Umoja wa sarafu ya Euro, pale ambapo chama kitakachochaguliwa kuiongoza serikali kitakapokataa kufuata maagizo ya kubana matumizi na kufanya mabadiliko ya sera.

Kiongozi wa chama cha EPP cha Ugiriki, Joseph Daul
Kiongozi wa chama cha EPP cha Ugiriki, Joseph DaulPicha: dapd

Lakini rais wa bunge la Umoja wa Ulaya, Bw. Martin Schulz, ameonya juu ya kufanya maamuzi kwa pupa. Yeye pia amevitaka vyama vya kisiasa vya Ugiriki kuunda serikali ya mseto itakayofuata masharti ya Umoja wa Ulaya. Umoja huo, kwa upande wake, unapaswa kuandaa programu ya kuleta ukuaji wa kiuchumi na kuongeza ajira kwa wagiriki.

Wazo hilo linaoana na wazo la Jorgo Chatzimarkakis ambaye ni mbunge wa cha kiliberali cha FDP cha Ujerumani katika bunge la Umoja wa Ulaya. Mwanasiasa huyo, mwenye asili ya Kigirki, ameiambia Deutsche Welle kwamba si Ugiriki tu, bali hata Ufaransa, Uhispania na Ireland zinazohitaji mpango kabambe wa kukuza uchumi.

Mwandishi: Christoph Hasselbach

Tafsiri: Elizabeth Shoo

Mhariri: Othman Miraji