Umoja wa Ulaya na Haki za Binadamu
10 Mei 2008Hizo ni lawama zilizotolewa katika ripoti mpya ya Bunge la Umoja wa Ulaya.Ripoti hiyo ya mwaka kuhusu haki za binadamu duniani, imeidhinishwa na Bunge la Umoja wa Ulaya mapema mwezi Mei.Inasikitika kuwa ingawa demokrasia na kuheshimiwa haki za binadamu ni msingi unaohifadhiwa katika sheria ya Umoja wa Ulaya,bado kuna haja ya kufanya maendeleo makubwa ili kuhakikisha kuwa sera hizo zinaheshimiwa.
Kwa maoni ya Marco Cappato alietayarisha ripoti hiyo,mara nyingi Umoja wa Ulaya unapotaka kutoa ujumbe mzito kuhusu haki za binadamu,juhudi hizo hukwama kwa sababu maslahi ya mataifa wanachama hutawala.Hali hiyo ilidhihirika mwezi Aprili,pale mawaziri wa nje wa Umoja wa Ulaya walipoamua kuondosha vikwazo vilivyowekwa na umoja huo dhidi ya Uzbekistan baada ya raia wasio na silaha kuuawa katika mwaka 2005.Vikwazo hivyo viliondoshwa ingawa hadi hivi sasa,hakuna uchunguzi rasmi usio na upendeleo uliofanywa.Ujerumani,nchi yenye wakaazi wengi katika Umoja wa Ulaya ilikuwa ikishinikiza kuondosha vikwazo hivyo.Ujerumani ina kituo cha kijeshi katika mji wa Termez kusini mwa Uzbekistan.
Mbunge Cappato katika ripoti yake amefahamisha kuwa upo utaratibu wa kuingiza masharti ya kuheshimu haki za binadamu katika mikataba ya biashara na ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na nchi za kigeni.Juu ya hivyo umoja huo hauna mwongozo wa kuhakikisha kuwa mikataba hiyo itaahirishwa,kunapotokea ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.
Ikiendelea ripoti hiyo ya mwaka inazishauri serikali za nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya na hata Halmshauri ya Ulaya kutayarisha orodha ya nchi zinazotia wasiwasi kuwa juhudi za kuendeleza haki za binadamu ziko mashakani.Vile vile uwepo utaratibu wa kupima maendeleo ya nchi fulani ili Umoja wa Ulaya ufahamu wapi shughuli zake kuhusu haki za binadamu zitahitaji kupewa kipaumbele.
Licha ya ukosoaji mkali,Cappato amesema,juhudi za Bunge la Ulaya lenyewe kuhusika na haki za binadamu zinaonyesha mafanikio.Kwani Bunge hilo kwa kupinga vikali adhabu ya kifo,limechangia kuzihimiza serikali za Umoja wa Ulaya kuunga mkono wito uliotolewa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Desemba mwaka jana,kupiga marufuku adhabu ya kifo.