1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya kujadili uhusiano wake na China-Belarus

Sylvia Mwehozi
14 Januari 2022

Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya leo watajadili uhusiano baina ya muungano huo na China na Belarus katika siku ya pili ya mkutano usio rasmi unaoendelea katika mji wa Brest nchini Ufaransa. 

https://p.dw.com/p/45Wi2
Frankreich | EU Verteidigunsministertreffen | PK Josep Borrell
Picha: AFP via Getty Images

Katika siku ya kwanza ya mkutano huo, mawaziri wa mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya walijielekeza zaidi kwenye ushirikiano wa kiusalama ndani ya muungano huo, katika mazungumzo yaliyogubikwa na ongezeko la mvutano baina ya Urusi na Jumuiya ya Kujihami NATO.

Juhudi za kidiplomasia ndani ya wiki hii zilizolenga kupunguza mvutano, zilimalizika siku ya Alhamis bila ya mafanikio na badala yake wanadiplomasia katika shirika la usalama na ushirikiano la Ulaya – OSCE, walitoa onyo kali juu ya uwezekano wa kuongezeka kwa shughuli za kijeshi.

Mwenyekiti wa shirika hilo na waziri wa mambo ya nje wa Poland Zbigniew Rau aliwaeleza waandishi wa habari mjini Geneva kuwa "inaonekana kuwa hatari ya vita katika eneo la OSCE sasa ni kubwa kuliko katika miaka 30 iliyopita,”.

Licha ya kauli hiyo, waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Annalena Baerbock alisema mazungumzo baina ya pande hizo mbili yanapaswa kusonga mbele. "Ingawa hapajakuwa na hatua kubwa kwa sasa ni muhimu kwamba hatimaye tunarejea katika meza ya mazungumzo", alisema waziri Baerbock mjini Brest.

Mwandiplomasia huyo wa Ujerumani ameongeza kwamba Umoja wa Ulaya una jukumu kubwa katika mazungumzo hayo ikiwa utasalia na sauti moja.

Siku ya Alhamis Umoja wa Ulaya uliweka vikwazo vipya dhidi ya Urusi kuhusiana na mgogoro wa mpaka na Ukraine. Uamuzi huo ulikuwa tayari umekubaliwa mwezi Desemba.

Österreich | OSZE-Sitzung im Zeichen der Krisendiplomatie mit Russland
Mkutano wa shirika la OSCE mjini ViennaPicha: Alexey Vitvitsky/Sputnik/dpa/picture alliance

Mwanadiplomasia wa juu wa Umoja wa Ulaya Josep Borell amesisitiza baada ya siku ya kwanza ya mazungumzo ya huko Ufaransa kwamba Umoja huo na Marekani zinashirikiana kwa karibu katikati mwa mvutano unaohusu kupelekwa wanajeshi wa Urusi katika mpaka wa Ukraine.

"Siku hizi, pamoja na Marekani, tumekuwa na uratibu wa hali ya juu sana. Tuko katika uratibu wa karibu, na tuna uhakika kwamba hakuna kitakachoamuliwa au hata kujadiliwa na Warusi bila uratibu wa karibu na Ulaya na bila ushiriki wa watu wa Ulaya"

Ufaransa ambayo kwa hivi sasa inashikilia urais wa kupokezana wa Umoja wa Ulaya, kwa muda mrefu imekuwa ikisisitiza juu ya kuongeza ushirikiano wa kijeshi ndani ya muungano huo.

Mawaziri hao pia watajadili hali ya sasa katika mpaka wa Belarus, ambako maelfu ya watu kutoka mataifa yaliyokumbwa na vita wamekwama kwa miezi kadhaa wakiwa na matumaini ya kuingia Ulaya.

Shinikizo la kiuchumi na kisiasa dhidi ya Lithuania ni miongoni mwa ajenda nyingine wakati mzozo wa kidiplomasia ukiendelea na Beijing. Wanadiplomasia wa Ulaya pia wataangazia fursa za kuimarisha mahusiano ya kimkakati kati ya Umoja wa Afrika na Ulaya kabla ya mkutano wa kilele mwezi Februari.