Umoja wa Ulaya kujadili mpango mpya wa wahamiaji
2 Septemba 2015Mamia ya wahamiaji waliozuiwa Hungary, wameandamana mbele ya kituo cha treni cha mashariki mwa mji mkuu wa Hungary, Budapest, leo hii, wakidai kupewa ruhusa ya kuingia ndani ya kituo hicho ili waelekee nchini Ujerumani huku wakiwa wanapiga makelele "Uhuru, Uhuru".
Zaidi ya wahamiaji 2,000 wakiwamo wanawake na watoto, walikuwa wanasubiri nje ya kituo hicho katika joto kali.
Msemaji mkuu wa serikali alipoulizwa kama Hungary itawapa ruhusa ya kusafiri na kueleeka Ujerumani wahamiaji hao kama walivyofanya siku ya Jumatatu, alisema Hungary itazingatia sheria za Umoja wa Ulaya.
Wahamiaji wazama Uturuki
Wakati huo huo vyombo vya habari vya Uturuki vimeripoti kuwa wahamiaji 11 wamefariki na wengine watano hawajulikani walipo baada ya boti mbili boti zilizokuwa zimebeba wahamiaji hao kuzama leo hii zikiwa njiani kuelekea kisiwa cha Kos Ugiriki.
Shirika la habari binafsi la Dogan limesema boti iliyobeba watu 16 ilizama, saba kati yao walikufa maji lakini wanne waliwahi kuokolewa.
Masaa machache baadae boti ya pili iliyokuwa na wahamiaji sita pia ilizama nje ya pwani ya Bodrum. Mwanamke mmoja na watoto watatu walizama, wakati wahamiaji wawili waliokuwa wamevaa vesti waliwahi kufika ufukweni lakini wakiwa hawana fahamu kamili.
Njia hiyo ya kutoka Bodrum Uturuki hadi kisiwa cha Kos cha Ugiriki ni njia fupi baina ya nchi hizo mbili, na ambayo maelfu ya wahamiaji wanaitumi licha ya kuwa ina hatari.
Kamishna wa uhamiaji wa Umoja wa Ulaya wenye nchi ishirini na nane Dimitris Avramopoulos amesema, watendaji wa Umoja huwo watapanga mipango mipya wiki ijayo ya kugawana wahamiaji baina ya nchi hizo. Pamoja na kuongeza kasi ya kuwasafirisha wahamiaji hao.
Kamishna huyo aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba mfumo mpya wa Umoja wa Ulaya kuhusu wahamiaji wanaomba hifadhi Italia, Ugiriki na Hungary utaanza kuwazuia wale walikataliwa hifadhi ya ukimbizi ndani ya nchi hizo hadi pale watakaporejeshwa nyumbani.
Katika majadiliano hayo, Avramopoulos amesema Halmashauri ya Umoja wa Ulaya itawasilisha mapendekezo yake kwa mawaziri wa mambo ya ndani katika mkutano wa dharura utakaofanyika Septemba 14. Siku tano baada ya Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker, anapotarajiwa kuwasilisha mipango ya bunge la Umoja wa Ulaya katika mkutano wa kila mwaka.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre/ape/rtre
Mhariri: Mohammed Khelef