Umoja wa Ulaya kuiwekea vikwazo zaidi Korea Kaskazini ?
9 Aprili 2013Wakati serikali ya Korea Kaskazini ikionya kwamba Rasi ya Korea inakabiliwa na vita vya nuklea na kuwashauri raia wa kigeni walioko Korea Kusini kufikiria kuondoka nchini humo afisa wa Umoja wa Ulaya amesema leo hii kwamba hali ni ya kutia wasi wasi lakini haihidhirishi iwapo uhasama huo utaripuka hivi karibuni.
Afisa huyo ambaye amekataa kutajwa jina lake amesema nchi saba za Umoja wa Ulaya ambazo zina ofisi zake za ubalozi katika mji mkuu wa Korea Kaskazini hazikuona maadalizi yoyote yale ya vita yakifanyika nchini humo na kwamba hazifikirii suala la kuondowa wafanyakazi wake wakati huu.
Wiki iliopita, Korea Kaskazini ilizitaka balozi hizo kufikiria kuwaondowa wafanyakazi ambapo Jumatano (10.04.2013) iwe imekwisha fanya hivyo kwani haitoweza kuhakikisha usalama wa wafanyakazi hao iwapo vita vitaripuka.Uingereza,Bulgaria,Jamhuri ya Czech,Ujerumani,Poland, Romania na Sweden zina ofizi za ubalozi katika mji mkuu wa Pyongyang.
Hivyo kweli hakuna dalili za maandalizi ya vita ?
Korea Kaskazini katika miezi ya hivi karibuni imekuwa ikichochea vita vya maneno kwa madai kwamba Marekani ilikuwa inapanga kuishambulia nchi hiyo na kwamba iko tayari kutumia silaha za nuklea.Afisa huyo mwandamizi wa Umoja wa Ulaya amesema umoja huo umekuwa ukifiuatilia kwa makini hali hiyo tete sana na kwamba nchi wanachama zinaangalia vikwazo gani zaidi inaweza kuiwekea nchi hiyo.
Umoja wa Ulaya iliweka vikwazo kwa kuzingatia idhini ya Umoja wa Mataifa kufuatia jaribio la kombora la masafa marefu la Korea Kaskazini hapo mwezi wa Disemba na jaribio lake la tatu la bomu la nuklea hapo mwezi wa Februari.Vikwazo hivyo vinapiga marufuku biashara ya vitu na mali ghafi ambazo zinaweza kutumika katika kutengeneza silaha na imeweka marufuku ya safari na kuzuwiliwa kwa mali za watu 26 wa Korea Kaskazini na taasisi zake 33.
Serikali ya Marekani imekuwa ikishinikiza pia kuwekewa vikwazo kwa Benki ya Biashara ya Korea Kaskazini ili kupunguza nafasi ya Korea Kaskazini kuweza kujipatia fedha za kigeni ambazo zinawasaidia kugharimia mpango wake wa nuklea.
Hali ni ya hatari sana
Akizungumzia hali hiyo leo hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema kwamba hali ya mvutano iliopo hivi sasa ni ya hatari sana na kwamba jambo dogo tu linaweza kuiripua hali hiyo na kuifanya ishindwe kudhibitika.Amesema amezihimiza nchi husika na zile zilioko karibu na Rasi ya Korea kutumia ushawishi wao kwa uongozi wa Korea Kaskazini.Ban amesema tayari amezungumza na uongozi wa China na kwamba atalizungumzia jambo hilo na Rais Barack Obama hapo Alhamisi.
Ban pia ameitaka Korea Kaskazini kukifunguwa kituo cha viwanda cha Kaesong kwa kusema kwamba ni mojawapo ya miradi yenye mafanikio makubwa kabisa kati ya Korea Kaskazini na Kusini na kwamba inaweza kusaidia kujenga uhusiano kati ya nchi hizo.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP
Mhariri : Josephat Charo